Ukarabati wa barabara katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakamilika

HomeKitaifa

Ukarabati wa barabara katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakamilika

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) limesema limekamilisha ukarabati wa awali wa barabara na maeneo yalioathiriwa na mvua za El Nino katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambazo zilizuia baadhi ya shughuli za utalii kufanyika katika hifadhi hiyo.

Itakumbukwa kuwa miezi michache iliyopita Tanzania ilishuhudia uharibifu mkubwa wa nyumba, madaraja na barabara kutoka na mvua za El Nino zilizoanza kunyesha mwezi Oktoba mwaka huu.

Kutokana na mvua hizo, takribani kilomita 2,407 za barabara za udongo na kilomita 769 za changarawe katika hifadhi ya Serengeti zilijaa maji na kuzuia baadhi ya shughuli za kitalii kuendelea ikiwemo usafirishaji.

Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi, aliyekuwa akizungumza na wanahabari jana Machi 10, 2024 jijini Dodoma  amesema kwa sasa barabara hizo za hifadhi ya Serengeti ambayo ni miongoni mwa hifadhi kubwa nchini zinapitika na watalii wataendelea kupatiwa huduma kama iliyokuwa awali.

“Tanapa katika hatua za awali imekamilisha matengenezo na sasa barabara hizo zinapitika na watalii wanaendelea kupata huduma zinazostahili,” amesema Matinyi.

Huenda marekebisho hayo katika hifadhi ya Serengeti yakapaisha zaidi idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo ambapo hadi kufikia mwezi Februari mwaka huu watalii milioni 1.4 walitembelea hifadhi hiyo.

Idadi hiyo ya watalii waliongia nchini ni asilimia 0.04 zaidi ya lengo lililowekwa na Serikali la kupokea watalii milioni 1.3 hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu.

Aidha, Matinyi amesema kwa sasa Tanapa  inatafuta njia mbadala wa kuhifadhi barbara hizo ikiwemo kuzijenga kwa lami ngumu na zege ili ziweze kustahimili mvua na mabadiliko ya hali ya hewa yanayoweza kutokea pia kutokana na kuadimika kwa malighafi ya changarawe.

error: Content is protected !!