Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema sensa ya mwaka 2022 itakuwa tofauti na sensa zilizopita, hususan kwa namna itakavyosaidia kupatikana kwa idadi ya makazi
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mkakati wa Uhamasishaji na Uelimishaji wa Sensa ya Watu na Makazi jijini Dodoma leo hii, Rais Samia amesema “Tangu tumepata uhuru nchi yetu haijawahi kufanya sensa ya majengo. Licha ya kwamba zilizopita zilikuwa zinaitwa sensa za watu na makazi lakini hatukuwa tukichukuwa idadi ya majengo na makazi ya watu. Aidha, Serikali sasa hivi ipo kwenye zoezi la utekelezaji wa mradi wa makazi, lakini mradi huu haukuwa unaenda vizuri na zoezi hili litakwenda kuweka hamasa kwenye zoezi lile,”
Aidha, Rais Samia alieleza kwamba sensa ya mwaka 2022 itaboresha miradi ya makazi inayoendelea nchini, ikiwa ni pamoja na tozo ya majengo.
Amesema “Tumeweka tozo ya makazi, lakini hatukuwa na idadi sahihi ya nyumba na makazi ya Watanzania nchini kwa hiyo zoezi hili litakwenda kutupa ubora huo na kujiamini kwamba tunafanya kazi kwa kujua anuani za makazi na idadi ya nyumba na aina za nyumba zilizopo.”
Sensa ya Watu na Makazi itafanyika mwezi Agosti mwaka 2022 huku ikitarajiwa kutumia zaidi mifumo ya kidijitali kuliko sensa zilizopita.