UVIKO-19: Wizara ya Afya yasema kuna ongezeko la maambukizi lakini hakuna wimbi la nne

HomeKitaifa

UVIKO-19: Wizara ya Afya yasema kuna ongezeko la maambukizi lakini hakuna wimbi la nne

Kufuatia kuwepo kwa mjadala kuhusu kauli ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwamba Tanzania hakuna wimbi la nne la ugonjwa ‘Corona’ pamoja na kauli ya Katibu Mkuu wa Wizaraya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Profesa Abel Makubi kwamba Tanzzania kuna ongezeko la maambukizi ya ugonjwa huo, Wizara ya Afya imetoa tamko.

Katika taarifa iliyotolewa jana Desemba 20, 2021 na Profesa Abel Makubi (Katibu Mkuu-Afya), Wizara imesema kauli ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwamba Tanzania hakuna wimbi la nne la UVIKO-19 ni sahihi, na pia kauli ya kwamba kuna ongezeko la maambukizi ni sahihi.

“Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imebaini taarifa za upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii, kati ya taarifa iliyotolewa na Waziri Mkuu kwamba hakuna wimbi la nne la UVIKO-19 na ile iliyotolewa na Katibu Mkuu Afya kuhusu kuongezeka kwa maambukizi ya UVIKO-19.

Kimsingi taarifa zote hizi ni sahihi na wala hazipingani kabisa. Hii ni kwa kuwa, kuongezeka kwa maambukizi au Visa hakumaanishi kuwa tayari ni wimbi jipya la maambukizi na kitaalamu hii hujulikana kama resurgence of new cases (kuongezeka kwa maambukizi mapya).

Kwa tafsiri halisi iliyotolewa na Stephen X. Zhang et al kwenye Jarida la Risk Management Health Policy la tarehe 13 Septemba 2021 “wimbi ni tofauti na ongezeko linalotokea ghafla na kwa kipindi kifupi (resurgence); ili kusema kuna wimbi jipya ni lazima hali ya ongezeko iendelee kwa kipindi fulani (walau kati ya siku 14-21)”.

Hivyo, kwa maelezo haya ya kitaalamu wananchi wapuuze upotoshaji wa taarifa sahihi za viongozi wote wawili na zimetolewa kwa wakati tofauti kama mwendelezo wa Serikali kuwasiliana na Umma.

Aidha, wananchi wanakumbushwa kuendelea kuchukua tahadhari na kujikinga kwani ugonjwa wa UVIKO-19 bado upo na maambukizi yamekuwa yakiongezeka. Wizara inaendelea kufuatilia mwenendo wa ugonjwa huu na itakuwa inatoa taarifa kulingana na mabadiliko kadri yanavyotokea kwa mujibu wa takwimu za kila siku.” taarifa hiyo imeeleza.

error: Content is protected !!