Katika kipindi cha Julai hadi Machi mwaka wa fedha 2024/2025, Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kunufaika na uwekezaji wa waendeshaji binafsi, hatua iliyozidi kuimarisha utendaji na kuongeza tija katika huduma za bandari hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), gharama za uendeshaji wa bandari zimepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na ushiriki wa kampuni binafsi, ikiwemo DP World na TEA Group Tanzania Limited (TEAGTL). Kupungua kwa gharama hizo kumechochea ufanisi na kuvutia zaidi meli kufanya shughuli zake kupitia bandari hiyo.
Aidha, mapato ya forodha yaliyokusanywa na TPA yameongezeka na kufikia shilingi trilioni 8.256, ikiwa ni ongezeko kutoka shilingi trilioni 7.082 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2023/2024. Hili ni ongezeko la zaidi ya trilioni 1.1, linaloashiria mafanikio makubwa ya kiutendaji na kiuchumi.
Kwa upande wa ajira, jumla ya Watanzania 764 wamepata ajira za moja kwa moja kupitia kampuni hizo binafsi, ikiwa ni sehemu ya matokeo chanya ya uwekezaji unaoendelea kufanyika katika sekta ya bandari.
Vilevile, muda wa meli kusubiri nangani umepungua kwa kiasi kikubwa, hatua ambayo imeondoa kabisa msongamano wa meli za makasha na kuongeza ufanisi wa upokeaji na upakuaji wa mizigo bandarini.
Uwekezaji huu umeonesha kuwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi unaweza kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo na maboresho ya miundombinu ya kimkakati nchini. Serikali inaendelea kusisitiza dhamira yake ya kuhakikisha bandari za Tanzania zinakuwa na ushindani wa kimataifa na kuchangia kwa kiwango kikubwa pato la taifa.