Kiongozi wa Chama cha Upinzani cha ACT Wazalendo nchini Tanzania Zitto Kabwe, amenukuliwa mara kadhaa kupita mitandao ya kijamii, akisema kwamba Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani, Freeman Mbowe ni Mfungwa wa Kisiasa.
Tarehe 21 Julai 2021 Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Aikaeli Mbowe alimatwa na polisi kwa shutuma za makosa ya ugaidi ikiwemo kuchoma moto vituo vya mafuta, pamoja na njama za kuua viongozi wa Serikali. Ni takribani miezi mitano sasa tangu kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani akamatwe na jeshi la polisi.
Wanaharakati wa kupigania Demokrasia nchini pamoja na wafuasi wa CHADEMA, wamekua wakifanya kampeni usiku na mchana kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, kuiambia Dunia kuwa Mbowe sio Gaidi, hivyo shutuma zote zilizo juu yake ni za kutengeneza na zenye lengo la kumdhoofisha kisiasa.
“Niikumbushe serikali kuwa mashtaka yasiyo na dhamana si mbinu mpya ya kudhibiti washindani wa kisiasa, ni mbinu ambayo imetumika ndani ya miaka 6 iliyopita na serikali za CCM kuwaziba midomo wote ambao hawakubaliani na nao kisiasa, ni mbinu ya kutesa watu,” amesema Zitto.
Lakini Freeman Mbowe kuwa mwanasiasa, kunamfanya kuwa mfungwa wa kisiasa?
Mfungwa wa Kisiasa ni nani?
Bado hakuna tafsiri ya mfungwa wa kisiasa inayokubalika ulimwenguni kote, ingawa ipo ambao kulingana na utafiti, hutumika kutoa tasfiri ya neno hilo.
Kwa mujibu wa RadioFreeEurope/RadioLiberty, Mfungwa wa Kisiasa (Political Prisoner) ni mtu aliyefungwa kutokana na shughuli zake za kisiasa, hasa ni yule mtu ambaye anakosa shughuli za Serikali yake kwa uwazi na bila hofu.
October 2012, Mkutano wa Baraza la Wabunge Ulaya (Parliamentary Assembly of the Council of Europe – PACE) ilikuwa taasisi ya kwanza isiyo ya kiserikali duniani kupitisha vigezo ambavyo vinahalalisha mtu kuitwa mfungwa wa kisiasa. Kwa mujibu wa PACE, mfungwa wa kisiasa lazima awe na vigezo vifuatavyo.
1. Kizuizi hicho kinakiuka uhakikisho wa kimsingi katika Mkataba wa Ulaya wa Haki za Kibinadamu, hasa uhuru wa mawazo, dhamiri, na dini; uhuru wa kujieleza na habari; na uhuru wa kukusanyika na kujumuika.
2. Kizuizini kimewekwa kwa sababu za kisiasa tu.
3. Urefu au masharti ya kizuizini hayalingani na kosa.
4. Anawekwa kizuizini kwa njia ya ubaguzi ikilinganishwa na watu wengine.
5. Kuzuiliwa huko ni matokeo ya kesi za kimahakama ambazo kwa wazi si za haki na zinazohusiana na nia ya kisiasa ya mamlaka.
Hivyo ni vigezo vya PACE, na hutumika katika mataifa yao tu. Hivyo basi, kwa Tanzania kumuita mtuhumiwa mfungwa wa kisiasa tunatumia kanuni na sheria gani? Wapo wafungwa waliofungwa kwa kesi mbalimbali kama uhujumu uchumi, rushwa, ufisadi na kadhalika, lakini katika historia ya taifa tu, tumeshawahi kuwa na mfungwa kisiasa?
Unaweza ukasema Bi. Titi Mohammed labda aliwahi kuwa mfungwa wa kisiasa, lakini Bi. Titi alifungwa kwa makosa ya uhaini. Hoja hapa ni kwamba, bado hatuna msingi thabiti wa kutambua nani wa kuitwa mfungwa wa kisiasa na asiyestahili jina hilo.
Ni nani anachagua fulani kuwa Mfungwa wa kisiasa?
Kwa mujibu wa PACE, nchi wanachama wa PACE wanaweza kuchagua wenyewe, vigezo gani vitumike kwa mtu kuitwa mfungwa wa kisiasa.
Amnesty International pia hutumia neno “mfungwa wa kisiasa” kuelezea mfungwa yeyote ambaye kesi yake ina kipengele cha kisiasa — ama katika motisha ya kitendo cha mfungwa, kitendo chenyewe, au motisha ya mamlaka katika majibu yao.
Shirika la Amnesty International halitumii sana neno la “Political Prisoner”, bali hutumia neno la “Prisoner of Conscience”.
Ingawa mashirika ya haki za binadamu duniani kama Shirika la Msalaba Mwekundu, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya yanapokea mapendekezo kutoka kwa taasisi ndogo na asasi za kiraia zinafanya za kulinda haki za binadamu kutoka kwenye mataifa husika juu ya vigezo vya mtu kuitwa mfungwa wa kisiasa. Ingiwa, ni ngumu kufanya hivyo kutokana na mataifa mengi kukosa mwongozo maalumu katika namna ya matumizi ya neno hilo (Polical Prisoner), na kwa mtu gani hasa, hivyo hulazimika kutumia vigezo vilivyowekwa na PACE.
Ingawa, mashirika mengi ya haki za binadamu duniani hukwepa sana matumizi ya neno la “Politcal Prisoner”, bali hutumia “Human Rights Defender”
Sasa Mbowe ni Polical Prisoner au Prisoner of Conscience?
Prisoner of Conscience – Ni yule mtu aliyefungwa au uhuru wake kukwapuliwa na dola kutokana na misimamo yao ya kisiasa, imani ya dini, kabila, jinsia, rangi, lugha, kipato cha uchumi na imani yake juu uchaguzi wa jinsia yake.
Je, Mbowe amekatwa kwa kosa gani? Katika ya hivyo vipengele vilivyotajwa hapo juu ni kipengele gani kinashabiiana na kesi ya Mbowe? So tunafahamu ni kwa makosa gani Mh. Mbowe anatiwa nayo hatiani. Kwa sasa, tuwe na akiba ya maneno kusubiri Jamhuri kuthibitisha tuhumu dhidi ya Mbowe na upande wa utetezi wa Mbowe kukanusha tuhuma hizo.
Lakini watu ambao wamekuwa wakichochea vurugu, ghasia na mapigano, hata kama ikiwa kufanya hivyo ni kupigania haki zao, basi hawastahili kuitwa “Prisoners of Conscience”, hii ni kwa mujibu wa Amnesty Internation. Kwa maana hiyo, Freeman Mbowe anaweza kukosa haki ya kuitwa mfungwa wa kisiasa kutokana na sababu hiyo, na hizi zifuatazo:
1. Kwanza Tanzania sio miongoni mwa mataifa ambayo yanaunda umoja wa PACE, mataifa ambayo yanamwongozo maalumu ambao huutumia kutambua wafungwa wa kisiasa.
2. Mbowe amekamatwa kwa shutuma za ugaida ikiwemo kupanga njama ya kudhuru viongozi wa kisiasa na kuchomo moto vituo vya mafuta. Hivyo basi, anakosa haki pia ya kuitwa Mfungwa wa Kisiasa au Prisoner of Conscience.
Lakini mkasa wa Mbowe bado ni kizungumkuti kumwita au kutomwita mfungwa wa kisiasa kutokana na namna Mbowe anavyopambanua na kujitambulisha kwa watu. Mbowe ni Mwanasiasa, hivyo ni ngumu sana kumtenganisha yeye na harakati zake za kuibana na kuikosoa Serikali waziwazi. Hivyo basi, kila ilivyo kukamatwa kwake lazima kwa namna moja au nyingine, kuhusishwe na maisha yake ya kisiasa hivyo kufanya aitwe Mfungwa wa Kisiasa.
Lakini kwa mtu kuitwe mfungwa wa kisiasa ni lazima kuwepo msingi wa tafsiri utakao utakaotokana na kanuni maalumu ili kutoa tofauti katia ya mfungwa mwingine na mfungwa wa kisiasa.
Hitimisho
Kwa kutumia vigezo vya PACE, Mbowe anaweza kuwa Mfungwa wa Kisiasa endapo tu Jamhuri itashindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yake. Lakini pia Mbowe anaweza asiwe Mfungwa wa kisiasa kama ikiwa tuhuma dhidi yake zikithibitika kuwa za kweli.
Lakini Tanzania hakuna Mfungwa wa Kisiasa, ni neno linatumika kulingana na mazoea ya kesi ya aina ya Mbowe zinazotokea katika mataifa mengine. Tumeona kwamba mataifa ya Ulaya yanao mwongozo maalumu kwa kutambua wafungwa wa kisiasa kuwatoutisha na wafungwa wengine, na hiyo huyasaidia mashirikia ya kimataifa kuwapigania haki zao na kuhakikisha wanaachiliwa pasi na masharti.
Kesi ya Mbowe kwa mujibu sheria, Mbowe ameshitakiwa kama mtu mwingine. Lakini nafasi yake katika jamii, chama chake, taifa na harakati zake za kuikosoa serikali na kuiwajibisha kama mwenyekiti, zinatia ukakasi na ugumu wa kuthubutu kusema Mbowe sio mfungwa wa kisiasa.
Hata hivyo, Mfungwa n mtu ambaye tayari mahakama imetoa uamuzi wa kifungo chake. Hivyo basi, kwakuwa bado hukumu ya Mbowe haijatolewa na mahakama kwamba anakwenda Gerezani, hivyo Mbowe anakosa hadhi ya kuitwa Mfungwa Kisiasa. Mbowe sio mfungwa, Mbowe bado ni mtuhumiwa, yuko mahabusu.
Dhana ya mfungwa wa kisiasa iko kikanuni na taratibu, ni zaidi ya kutamka tu kutokana na harakati za mtu kwenye siasa au kuwa mwanasiasa. Sio kila mwanasiasa anaweza kuwa mfungwa wa kisiasa, bali mtu yeyote anaweza kuwa mfungwa wa kisiasa, lakini lazima kuwe na kanuni na taratibu kama zile za PACE ambazo kiuhalisia, Tanzania bado hatuna.