Viongozi wa Kanda CHADEMA mkoa wa Mwanza na wanachama 170 watimkia CCM

HomeSiasa

Viongozi wa Kanda CHADEMA mkoa wa Mwanza na wanachama 170 watimkia CCM

WANACHAMA 170 wapya wamejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mwanza, Peter Machoko.

Wengine ni Katibu Mwenezi wa Kanda ya Victoria, Omary Mtua na wajumbe wa Kamati ya Utendaji kanda na Mkoa wa Mwanza.

Wanachama hao wamepokelewa Mei 2,2025 na Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Furahisha mkoani Mwanza.

Makalla ameahidi CCM itawapa wanachama hao ushirikiano Mkubwa kwani wamejiunga na CCM katika kipindi muafaka ikiwa katika maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu na jeshi hilo la watu 170 ni chachu na nguvu kubwa kwa CCM.

“Nitasema takwimu hapa wale wa kwanza walikuwa 135, jawa wakubwa watano tunapata 140 na vijana 30 tunapata 170 wamejiunga na Chama Cha Mapinduzi taratibu zifanyike za kuwapatia kadi za CCM,” amesema Makalla.

Aidha, Makalla amepongeza na kuwashukuru wananchi na wana CCM Mkoa wa Mwanza kwa kukipa chama hicho ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana.

Makalla amesema ombi lao walipopita mwaka jana akiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi na wajumbe wa Sekretarieti ya chama ni kuahikikisha Mwanza yote inakuwa ya kijani na imekuwa hivyo.

Ameongeza kuwa ushindi huo umetokana na imani kubwa ya wananchi kwa CCM kwakuwa kinadhamana ya kuwaletea wananchi maendeleo.

error: Content is protected !!