Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa kwenye sekta ya Afya hususani Ujenzi wa Vituo 10 vya Afya kwenye Mkoa huo vilivyogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 5 ikiwa ni matunda ya fedha zitokanazo na tozo ya miamala ya simu.
RC Makalla amesema hayo wakati wa Maadhimisho ya siku ya Fiziotherapia Duniani yaliyofanyika Hospital ya Taifa Muhimbili ambapo amesema Ujenzi wa Vituo hivyo umesaidia kutatua changamoto ya Wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma.
Kuhusu tiba ya Fiziotherapia RC Makalla amehimiza Elimu ya mkao maofisini na kunyanyua vitu vizito kutolewa kwa Wananchi kwakuwa imekuwa moja ya visababishi vya maumivu ya shingo na mgongo na kufanya kushindwa kuhudhuria kazini kila siku.
Pamoja na hayo RC Makalla ametoa wito kwa hospital ya Taifa Muhimbili kupitia idara ya Fiziotherapia kufanya tafiti za kupata takwimu halisi za Wakazi wa Dar es salaam ambao Wana matatizo hayo na kutoa ushauri wa namna ya kuyakabili.
Hata hivyo RC Makalla ameitaka Jamii kuacha tabia ya kuwaficha watoto Wenye matatizo ya kuchelewa Makuzi na badala yake wawapeleke hospital ili kupata tiba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru amesema hospital hiyo imekuwa ikipokea takribani Wagonjwa 150 Hadi 200 kwa siku wakiwemo watoto waliochelewa makuzi na watu Wenye maumivu ya shingo, mgongo na magoti.