Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetangaza kuwa vituo vya gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) zaidi ya 12 vitakuwa vinafanya kazi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Hatua hiyo ni juhudi kubwa katika kuelelea matumizi ya nishati safi na kupunguza misururu ya magari katika vituo vya mafuta.
Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), Mhandisi Mwandamizi kutoka Kampuni Tanzu ya Gesi ya TPDC (GASCO), Hassan Temba alisema hatua hiyo ni fursa ya kipekee kwa watumiaji nchini.
Alisema utekelezaji wa mpango huo unaongozwa GASCO.
“Tunashukuru dhamira ya TPDC ya kupanua miundombinu ya CNG, tayari vituo vinane vinafanya kazi na vituo vinne viko katika hatua za mwisho za ukamilishaji,” alisema Temba.
Alisema maendeleo hayo yanatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari katika vituo vya gesi vilivyopo na kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi.
Temba alisema vituo vya Mbezi-Tangi Bovu, IPTL na Goba vimekamilika kwa zaidi ya asilimia 80 na kilichobaki ni kazi ndogo ya miundombinu kabla ya kuanza kutoa huduma kwa wateja.
Kwa mujibu wa Temba, mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa tangu uzinduzi wa kituo cha kwanza cha CNG cha TPDC, huku idadi ya watumiaji wa gesi hiyo ikizidi kuongezeka.