Wananchi wanaoishi katika Kijiji cha Kipenjiro, Kata ya Naiyobi katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, wameomba serikali iharakishe mchakato wa kuwahamisha waondokane na tatizo la kuvamiwa na wanyama wakali hususani watoto wanaotembea umbali mrefu kwenda shuleni.
Wananchi hao walisema wanatamani maisha ya wenzao wanaoishi Msomera mkoani Tanga ambako hakuna wanyama na badala yake wanaishi kwa uhuru na kufanya shughuli zao bila wasiwasi.
“Huku Ngorongoro mifugo yetu inaliwa na wanyama wakali, lakini tukiwasiliana na wenzetu walioenda Msomera wanasema maeneo ya malisho yapo na hakuna mifugo inayoliwa na wanyama huko, sasa kwa nini tuendelee kukaa hapa ambapo wanyama wakali wanaingia kwenye mazizi au katika malisho kula mifugo yetu,” alisema Saruni Parokie, mmoja wa wanakijiji cha Kipenjiro.
Parokie alisema: “Tupo tayari kuondoka hata sasa ili kwenda Msomera kuishi na kulisha mifugo yetu kwa amani.”