Ramadhani Kingai ameteuliwa kuwa DCI na Rais Samia Suluhu Hassan, Jumanne usiku, Julai 19,2022 akichukua nafasi ya Camilius Wamabura ambaye ameteuliwa kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania (IGP).
Kabla ya uteuzi huo, Kingai alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma wadhifa ambao amehudumu kwa siku nne tu.
Julai 15, 2022 ndipo alipohamishwa na aliyekuwa IGP, Simon Sirro kwenda mkoani humo, baada ya kuhudumu nafasi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Dar es Salaam tangu Januari 10, 2021 alipochukua nafasi ya Edward Bukombe.
Kingai aliwahi kuwa Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi hilo Mkoa wa Arusha ambapo kabla alikuwa Naibu Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Pia, aliingia katika ushahidi wa kesi iliyokuwa inamuhusu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe kutokana na nafasi yake ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha aliyokuwa nayo wakati huo.