Huenda itakuwa tabasamu kwa wanafunzi wanaotarajia kusoma masomo ya lugha ikiwemo Kiswahili katika vyuo vikuu baada ya Serikali kutangaza kuyapa kipaumbele masomo hayo katika maombi ya mikopo mwaka 2022/23.
Miaka ya nyuma masomo hayo yalikuwa hayapewi kipaumbele huku masomo ya sayansi na ualimu ndiyo wanafunzi wake walikuwa wakinufaika zaidi na mikopo hiyo ya elimu ya juu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema lengo la kutoa mikopo zaidi kwa masomo hayo ni kuchochea ongezeko la wahitimu wa masomo ya lugha na ukalimani Tanzania.
“Baada ya dunia kuadhimisha siku ya Kiswahili na kwa msisitizo ambao Rais wetu (Samia Suluhu Hassan) ameuweka wa kukuza lugha yetu ya Kiswahili.
“Sasa kuanzia mikopo ya mwaka huu (2022/23) wale watakaosoma Kiswahili, ukalimani watawekwa katika kundi la kwanza kwa hiyo watapewa upendeleo mkubwa zaidi wa kupata mkopo ili wasome chuo kikuu,” amesema Mkenda.
Prof Mkenda aliyekua akizungumza wakati wa uzinduzi wa dirisha la maombi ya mkopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka 2022/23 katika ofisi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jijini Dar es salaam leo Julai 12, amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza wakalimani na watu wanaozungumza lugha zaidi ya moja ili kueneza Kiswahili ambacho Tanzania ndiyo kitovu chake.
Dirisha la maombi ya mikopo ya elimu ya juu linatarajiwa kufunguliwa Julai 19 mwaka huu na litakuwa wazi hadi Septemba 30 ambapo wanafunzi wataruhusiwa kuwasilisha maombi ya mkopo kwa njia ya mtandao.
Kipaumbele cha kwanza masomo ya lugha, huenda kikawavutia wanafunzi wengi kusoma masomo hayo na nchi ikanufaika na fursa za kimataifa za lugha ya Kiswahili ambayo inasambaa kwa kasi duniani.
Mwaka huu wa masomo Serikali imetenga Sh570 bilioni zitakazowafaidisha wanafunzi 205,000 huku wanafunzi 500 watapata ruzuku (sholarship) ya Sh3 bilioni.