Wakati dunia leo akiadhimisha siku ya Kimataifa ya Kusoma na Kuandika, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) limesema hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2021, Watanzania milioni 5.5 walikuwa hawajui kusoma wala kuandika.
Unesco katika ripoti yake kuhusu kiwango cha kusoma na kuandika ya mwaka 2021 imeeleza kuwa idadi hiyo ya wasiojua kusoma na kuandika inahusisha watu wenye umri kuanzia miaka 15 na kuendelea.
Sababu kubwa inayotajwa ya changamoto hiyo ni kutokuwepo kwa miundombinu ya kutosha ya elimu ikiwemo madarasa na vitabu, jambo linalosababisha wanafunzi kukosa maarifa na ujuzi.
Siku ya Kimataifa ya Kusoma na Kuandika ya mwaka huu inaadhimishwa chini ya kaulimbiu, “Kubadilisha Nafasi za Kujifunza Kusoma na Kuandika” ili kufikiria upya umuhimu wa kimsingi wa nafasi za kujifunza kusoma na kuandika ili kujenga uthabiti na kuhakikisha elimu bora, sawa, na jumuishi kwa wote.
Unesco inaeleza kuwa takribani vijana na watu wazima milioni 771 hawana ujuzi wa kimsingi wa kusoma na kuandika duniani kote.
Kupitia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kusoma na Kuandika, Unesco inatoa wito kwa wahusika wote katika nyanja ya elimu na kwingineko kufikiria upya jukumu la kusoma na kuandika.
Ili kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma, wadau wanahitaji kuimarisha na kubadilisha nafasi zilizopo za kujifunza kupitia mbinu jumuishi na kuwezesha kujifunza kusoma na kuandika katika mtazamo wa kujifunza katika kipindi kirefu cha maisha.
SOURCE: NUKTA HABARI