Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, amewakemea wakandarasi wa mradi wa maji wa miji 28 unaotekelezwa Wanging’ombe na Makambako, mkoani Njombe, kutokana na ucheleweshaji wa kazi na kutoridhisha kwa utekelezaji.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Waziri Aweso amesema serikali ya awamu ya sita ina imani kubwa na wakandarasi wazawa, lakini utekelezaji wa sasa hauakisi thamani ya fedha wala matarajio ya wananchi.
Kwa sasa, mradi umefikia asilimia 47.3 pekee, chini ya lengo la asilimia 80, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Wanging’ombe, Mhandisi Fabian Maganga.
Waziri amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Antony Mtaka, kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi na kuchukua hatua kali kwa wote wanaokwamisha maendeleo, huku akiagiza wakandarasi kufanya kazi kwa saa 24 kurekebisha hali hiyo.
Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Larsen & Toubro LTD kwa kushirikiana na kampuni za ndani.