Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema chama hicho kimekubaliana na Rais Samia Suluhu Hassan kurejesha Taifa katika misingi inayojenga mshikamano kumaliza chuki na uhasama kiitukadi.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Sabasaba maarufu kama “Shamba la Bibi” mjini Tarime jana Jumatatu Januari 23, 2023, Mbowe amesema makubaliano hayo yana lengo la kuwapa wananchi haki, amani na furaha kwa kuondoa tabia ya Watanzania kuwindana na kujengeana chuki kwa msingi wa tofauti zao kiitikadi.
Kuhusu mapambano ya kisiasa ya chama hicho, Mbowe amesema lengo la chama chake ni kudai uhuru, haki, usawa na ustawi kwa Watanzania wote bila ubaguzi wa kiitikadi, cheo wala hali ya kiuchumi wa mtu.
“Demokrasia na haki ya watu kuchagua viongozi wao kutoka chama chochote cha siasa wanachotaka ni msingi mwingine wa mapambano yetu Chadema,” amesema Mbowe
Akizungumzia uchumi, kiongozi huyo amesema lengo la Chadema ambayo pia ilinadiwa kupitia sera na ilani ya uchaguzi mwaka 2020 ni kuona uongozi wa Taifa unajenga na kuimarisha uchumi ili hatimaye kuongeza kipato cha wananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Akihutubia mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amewasihi Watanzania kila mmoja kwa eneo na nafasi yake kupigania Katiba Mpya itakayowawajibisha wakati wowote viongozi wa umma wakiwemo madiwani na wabunge wanaoshindwa kutimiza wajibu badala ya kusubiri hadi miaka mitano imalizike.
“Haki ya wananchi kuwaita na kuwahoji madiwani na wabunge wasiowajibika ilikuwa moja ya maoni ya wananchi katika rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba lakini iliondolewa. Tunahitaji Katiba inayotoa mamlaka kwa wananchi kuwajibisha viongozi wao,” amesema Mnyika
Akizungumzia rasilimali za Taifa ikiwemo madini, Mbunge wa zamani wa Tarime vijijini, John Heche ameshauri sheria ya uwekezaji uweke masharti ya wananchi wanaoisha maeneo yenye madini kuingia ubia na wawekeza ili kunufaika moja kwa moja na utajiri huo badala ya utaratibu wa sasa wa kuondolewa kwa fidia isiyolingana na thamani ya madini iliyoko ardhini.
“Utaratibu huu utamaliza hali ya sasa ya maisha duni ya wananchi wanaoishi jirani au maeneo yenye utajiri wa madini,” amesema Heche