Ikiwa zimebaki siku chache kabla ya kufanyika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), yapo mambayo kadhaa yakajitokeza katika sherehe za mwaka huu.
Katika sherehe hizo zitakazofanyika kitaifa katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro zimeandaliwa na Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Hiyo itakuwa mara ya tatu kwa Rais Samia kuhudhuria sherehe hizo tangu aapishwe kuwa Rais wa sita wa Tanzania Machi 19 mwaka 2021 akichukua nafasi ya Hayati John Magufuli.
Kauli mbiu ya Mei Mosi ya mwaka huu wa 2023 ni “Mishahara Bora na Ajira za Staha ni Nguzo kwa Maendeleo ya Wafanyakazi. Wakati ni Sasa.”
Yanayotarajiwa siku ya mei mosi
Yafuatayo ni mambo kadhaa ambayo yanaweza kuteka ajenda za maadhimisho hayo na ambayo wafanyakazi wanayasubiri kuyasikia.
Kodi ya mishahara ya wafanyakazi
Katika sherehe za Mei Mosi mwaka 2021, Rais Samia alitangaza kupunguza kiwango cha kodi katika mishahara (PAYE) kutoka asilimia 9 ya wakati huo hadi asilimia 8 kilichoanza mwaka wa fedha wa 2021/22.
Hata hivyo, kwa mujibu wa viwango vya kodi vilivyopo sasa, punguzo hilo linawabeba zaidi wafanyakazi wa kada ya chini wanaolipwa mshahara unaozidi Sh270,000 hadi Sh520,000.
Lakini kwa wafanyakazi wanaolipwa mshahara zaidi ya Sh520,000 na kuendelea wanalazimika kulipa kodi ya ziada ukiondoa kodi ya msingi ya asilimia nane.
Kodi katika mishahara ya asilimia nane inayotumika sasa itapungua au itaongezeka? Tusubiri Mei Mosi.
Nyongeza na kima cha chini cha mishahara kitakuwepo?
Mwaka jana, Serikali ya Tanzania ilitangaza kupandisha kima cha chini cha mshahara wa wafanyakazi wa umma kwa asilimia 23.3.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyekuwa akizungumza Julai 29, 2022 jijini Dodoma alisema kuwa nyongeza ya mishahara iliwalenga zaidi wafanyakazi wanaopokea kima cha chini cha mshahara na siyo wafanyakazi wote.
“Ni kweli asilimia 23 iliyotamkwa haijalipa watu wote, na hii ni kwa sababu ya formula inayotumika katika kutamka viwango vya Mshahara. Inapotamkwa wanaonufaika si wote mpaka wa mishahara mikubwa, bali ni wale wa kada ya chini,” alisema Majaliwa.
Amesema wanaonufaika ni wale wa kada ya chini, ambao kwa tangazo la mwaka huu wanufaika ni asilimia 75 hadi 78 ya watumishi wote.
Amesema nyongeza hiyo itawafaidisha zaidi wafanyakazi wa kada ya chini ili wawezesha kuboresha maisha yao katika kipindi hiki ambacho karibu kila bidhaa imepanda bei, jambo linaloongeza ukali wa maisha.
Mwaka huu Serikali itawakumbuka wafanyakazi na kuwaongezea kima cha chini na nyongeza ya mshahara?
Madaraja ya wafanyakazi wa umma
Septemba 2022, Serikali iliwapandisha madaraja watumishi 262,800 ambao kwa miaka mitano walikuwa hawajapanda huku ikitumia Sh58.3 bilioni kulipa mishahara kwa watu waliopandishwa.
Pia aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama Oktoba 19, 2022 alisema katika mwaka huu wa fedha wa 2022/23 watumishi 120,210 wametengewa fedha ili wapandishwe madaraja.
Suala la upandishwaji madaraja/vyeo kwa watumishi wa umma linazingatia vigezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na utendaji kazi mzuri, kukidhi sifa zilizoainishwa katika miundo ya maendeleo ya utumishi, uwepo wa nafasi wazi na bajeti iliyotegwa.
Sherehe za Mei Mosi za mwaka huu kutakuwa na matumaini yoyote kwa wafanyakazi kupanda madaraja?
SOURCE: Nukta Habari