Utengenezaji wa jamu si mgumu sana kama ambavyo wengi hudhani. Unaweza kutengeneza jamu kwa kutumia vifaa ulivyonavyo jikoni kwako.
Jamu ya machungwa ama ‘orange marmalade’ ni moja ya jamu zenye virutubisho vingi vya afya ikiwemo vitamin C, nyuzinyuzi zenye kusaidia mmeng’enyo wa chakula, na kupunguza matatizo ya moyo.
‘Marmalade’ inaweza kutengenezwa kwa kutumia matunda ya jamii ya machungwa kama vile machenza, malimao, ndimu, na mengine mengi lakini hasa yenye uchachu ili kuleta ladha nzuri.
Viungo
Machungwa 2kg
Maji ya kutosha kiasi cha kutosha kufunika mchanganyiko wako.
Sukari 1.5kg
Malimao/ ndimu 2
Vifaa
Sufuria kubwa ya kutosha
Mfuniko wa sufuria
Kitambaa kisafi cha kuchujia sharubati
Bakuli 3, ya machungwa, sharubati
Ubao wa kukatia mboga
Chombo cha kuhifadhia
Upishi
1.Osha machungwa yako vizuri kuondoa uchafu wowote unaoonekana
2. Kata machungwa yako katika vipande vya nusu nusu kisha kamua sharubati kutoka kwenye machungwa na weka kwenye bakuli moja.
3. Tumia kijiko kutoa nyama za chungwa zilizobaki kwenye maganda unaweza kuacha mbegu ama kuzitoa kama machungwa yana uchachu unaofaa na kuweka kwenye bakuli ya pili.
Kwenye bakuli ya tatu weka maganda yako ya machungwa (usiyatupe)
3. Chukua maganda yako unaweza kutoa ule weupe wa ndani ya ganda kwa kisu ama ukamua kuucha kisha katakata maganda yako ya machungwa na kuyaweka kwenye sufuria yako kubwa
4. Mimina sharubati yako kwenye mchanganyiko wa maganda kisha weka maji hadi yafunike maganda kidogo.
5. Katakata limao au ndimu yako na kisha tia kwenye mchanganyiko wako.
6. Tenga sufuria jikoni na chemsha hadi maganda yalainike na maji yapungue.
7. Funga nyama za chungwa kwenye kitambaa chako na dumbukiza kwenye mchanganyiko wako unaochemka.
8. Mchanganyiko ukichemka epua sufuria kisha mimina sukari yako koroga hadi sukari yote iyeyuke.
9. Kamua maji yote kwenye kitambaa na kisha kitoe
10. Acha ipoe kisha rejesha tena sufuria jikoni weka moto mdogo na koroga hadi iwe nzito na mganda yawe malaini kiasi cha kukatika kwa kijiko na mchanganyiko wako mzito kiasi ukiweka kweny sahani haugandi lakini pia haumwagiki.
Epua na weka kwenye chombo cha kuhifadhia acha jamu ipoe tayari kwa matumizi.
Inaweza kukaa hadi miezi sita bila kuharibika kama itahifadhiwa vizuri.