Abdul Kasuku (16) mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Mpigimahoge amedaiwa kujinyonga kwa waya jana asubuhi katika shamba la mihogo na miembe jirani na nyumbani kwao.
Baba mzazi wa mtoto huyo, Yahya Kasuku alisema kabla ya tukio hilo alishangaa kuona mwanawe hajaenda shule licha la kupewa fedha kwa ajili ya matumizi pamoja na mdogo wake.
“Nilimuuliza mbona hujaenda shule akanijibu nitaenda, lakini baadaye mama yake akaniambia kuwa anatapika hata hivyo nilimkazia lazima aende shule nikiamini kutapika pekee hakuwezi kumfanya ashindwe kwenda shule,” alisema Kasuku.
Pia alisema baada ya kumueleza mwanawe yeye alienda ndani kupumzika akiamini atafanya hivyo, lakini ghafla mke wake alimuamsha na kumwambia mwanawe amejinyonga kwenye shamba.
“Baada ya kutoka kuja pale kweli alikuwa amejinyonga kwa kutumia waya alioufunga kwenye tawi la mti wa mwembe, akiwa bado anahangaika nikamshika miguuni na kumuambia mke wangu akate kamba lakini hata hivyo hatukufanikiwa kuokoa maisha yake,” alisema Kasuku.
Kasuku alitoa taarifa kwa mjumbe wa mtaa wa Mbezi Sukusi Kusini, Shomary Sengo ambaye pia alienda kujiridhisha na tukio hilo kabla ya kutoa taarifa polisi.