Aeleza namna bora ya kumuenzi hayati Mkapa

HomeKitaifa

Aeleza namna bora ya kumuenzi hayati Mkapa

Rais Samia Suluhu Hassan amesema njia bora ya kuendelea kumuenzi aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Benjamin Mkapa ni kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi hasa katika kuboresha afya za Watanzania.

Hayati Mkapa aliyekuwa Rais watatu wa Tanzania  kati ya mwaka 1995 hadi 2005  alifariki miaka miwili iliyopita ambapo katika uongozi wake alifanya mageuzi makubwa yaliyowezesha Serikali kufanya kazi kwa karibu na sekta binafsi.

Hata baada ya kustaafu Mzee Mkapa alianzisha Taasisi ya Benjamin Mkapa inayojikita katika uboreshaji wa afya ya mama na mtoto, wahudumu wa afya na miundombinu ya kutolea huduma za afya.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza leo Julai 14, 2022 katika kongamano la pili la kumuenzi Hayati Mkapa lililofanyika visiwani Zanzibar, amesema taasisi hiyo ni mfano bora wa taasisi binafsi zinazotoa mchango mkubwa katika sekta ya afya nchini.

“Kupitia taasisi hii kwa miaka 16 sasa, watumishi wa afya wa kada mbalimbali wapatao 10,041 wakiwemo kada za madaktari, wauguzi, matabibu, wafamasi pamoja na wahudumu wa afya ngazi ya jamii wamesambazwa kote nchini,” amesema Rais Samia.

Amesema watumishi hao wameongeza tija na ufanisi katika utoaji huduma bora za afya kwa wananchi wa Tanzania. 

Hata hivyo Rais Samia amesema bado ushirikiano wa sekta binafsi na Serikali katika baadhi ya maeneo hauko sawa, jambo ambalo linahitaji msukumo mpya ili kuwawezesha Watanzania kufaidika na ushirikiano huo.

“Bado wengi wetu tumeelemewa na kasumba ya kutoamini sekta binafsi hivyo kumbukizi hiyo iwe sehemu ya kuwakumbusha viongozi umuhimu wa mabadiliko,” amesema Rais.

Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema Hayati Mkapa alikuwa muasisi wa sera za sekta binafsi kufanya kazi kwa karibu na Serikali kupitia sera ya kubinafsisha mashirika ya umma kwa watu binafsi ili kuongeza ufanisi.

Amesema ikiwa sekta binafsi itafanya kazi kwa karibu na Serikali, hiyo ndiyo inaweza kuwa njia bora ya kumuenzi Mzee Mkapa ambaye aliipenda nchi na wananchi wake kwa kuhakikisha anawaboreshea huduma za afya.

Aidha, Rais Samia amesema anatarajia sekta binafsi itatoa ushirikiano kwa Serikali pamoja na kuzingatia kuwa afya ni hitaji la jamii hivyo wasiweke faida kama kipaumbele bali huduma ndio ipewe kipaumbele.

“Afya ni stahili ya umma na siyo biashara kwa asilimia 100, hivyo lazima mzingatie urali kati ya kupata faida kiasi na kuwekeza katika kutoa huduma endelevu za afya kwa jamii na kuwekeza pale kwenye mahitaji makubwa zaidi kwa maslahi ya umma,” Rais Samia amesisitiza..

error: Content is protected !!