Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba, pamoja na Balozi wa Tanzania kwenye nchi za Nordic, Mhe. Grace Olotu na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mhe. Elisabeth Jacobsen wameshiriki katika warsha ya viongozi iliyofanyika kwenye mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia (Liquefied Natural Gas Plant – LNG) wa Equinor. Mradi huo upo Kaskazini mwa Norway kwenye mji wa Hammerfest.
Warsha hiyo iliyowashirikisha pia Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Bw. Kheri Mahimbali na uongozi wa juu wa kampuni ya Equinor, ilitoa nafasi kwa viongozi hao kujadili maandalizi ya mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia Tanzania wenye thamani ya shilingi trilioni 70 utakaofanyika mkoani Lindi.
Viongozi hao walitumia fursa hiyo kukutana na wafanyabiashara wa eneo hilo wanaonufaika kwa kutoa huduma kwenye eneo hilo la mradi wa Equinor, Hammerfest. Pia kukutana na Watanzania wanaofanya kazi katika mradi huo.
Mtambo uliojengwa kwenye mradi huo wa Equinor huchakata bilioni 4.6 za mita za ujazo za gesi asilia kwa mwaka ikiwa ni pamoja na bidhaa nyingine kama gesi ya kupikia (LPG).
Waziri Makamba aliwahakikishia Equinor na washirika wake kuwa Serikali ya Tanzania, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, itaendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha kuwa majadiliano yote ya msingi kuhusu mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia nchini yanakamilika ifikapo Desemba mwaka huu.