Royal Tour Tanzania  yazinduliwa nchini Sweden

HomeKimataifa

Royal Tour Tanzania yazinduliwa nchini Sweden

Serikali ya Tanzania kupitia ubalozi wake uliopo Sweden imezindua filamu ya Royal Tour jijini Stockholm kwa lengo la kuwavutia watalii kutembelea vivutio mbalimbali hapa nchini.

Sekta ya utalii duniani ilipata pigo miaka ya karibuni baada ya kusambaa kwa Covid-19 lakini sasa Tanzania imekuja na mikakati mbalimbali, ikiwemo filamu ya Royal Tour, kwa lengo la kuichechemua.

Akizungumza kutoka Skockholm Sweden, Balozi wa Tanzania nchini humo, Grace Olotu amesema sherehe za uzinduzi wa filamu ya Royal Tour mjini Stockholm zilizofanyika hivi karibuni zilihudhuriwa na waandishi wa habari za utalii nchini humo ambao wanatarajiwa kuitangaza kwa soko la utalii la nchi hiyo.

Amesema uzinduzi wa Filamu hiyo iliyoandaliwa na mtaalam kutoka Marekani akiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inayoelezea  vivutio vya utalii vya Tanzania umefanyika kwa lengo la  kuitangaza ili kuwavutia watalii kutoka nchi tisa za Scandinavia na ukanda wa bahari ya Baltic.

Balozi Olotu amesema Serikali itaendelea na juhudi za kutangaza utalii kwa kuzindua filamu ya Royal Tour katika  nchi zote tisa anazozisimamia ikiwemo Norway, Finland, Denmak, Iceland, Lithuania, Istonia, Latvia, Ukraine na Sweden ambapo tayari uzinduzi huo umefanyika hivi karibuni.

“Nina matumaini makubwa kuwa juhudi za Serikali kupitia ubalozi wetu kwa kushirikiana na wadau wengine zitazaa matunda na kuongeza idadi kubwa ya watalii baada ya kipindi cha mpito ambapo nchi nyingi zilikabiliana na athari za UVIKO 19 katika sekta ya utalii,” amesema Balozi Olotu.

Akizungumzia Diplomasia ya Uchumi, Balozi Olotu amesema takwimu zinaonyesha nchi hizo zimewekeza kiasi cha dola za kimarekani bilioni 1  katika miradi mbalimbali 193 nchini  ambayo imeajiri takribani Watanzania 12,000.

Ametaja sekta ambazo nchi hizo zimewekeza kuwa ni pamoja na kilimo, utalii, usafirishaji, uzalishaji, maliasili, nishati, ujenzi na mawasiliano.

Amesema Serikali inaendelea kutekeleza sera yake ya Diplomasia ya Uchumi duniani  kwa kutangaza utalii, fursa za biashara na uwekezaji zilizopo  nchini.

error: Content is protected !!