Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua dirisha awamu ya nne na ya mwisho ya udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu litakalokuwa wazi kwa muda wa siku tano.
Dirisha hilo litakuwa wazi Oktoba 3 hadi 7, 2022.
TCU imefungua dirisha hilo kutokana na uwepo wa baadhi ya waombaji ambao hawakufanikiwa kupata udahili katika awamu zilizopita na vyuo ambavyo bado vina nafasi ya kuendelea na kudahili.
Taarifa hiyo iliyotolewa jana Oktoba 3, 2022 na TCU imewataka waombaji wa masomo ya elimu ya juu ambao hawakuweza kutuma maombi ya udahili au hawakufanikiwa kudahiliwa katika awamu zilizopita kutumia dirisha hil0 kutuma maombi yao ya udahili kwenye vyuo wanavyovipenda kabla ya Oktoba 7.
Aidha, katika taarifa hiyo TCU imewataka waombaji wa udahili wa shahada ya kwanza kuwasilisha masuala yote yanayohusu udahili au kujithibitisha kwenye vyuo husika.
“Kwa ambao watapata changamoto katika kujithibitisha, vyuo vyote vimeelekezwa kupokea taarifa zao na kutafuta ufumbuzi wa haraka kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizowekwa,” imesema taarifa hiyo.
Jitahadharisheni na upotoshaji
Kufuatia kuibuka kwa wimbi kubwa la upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu wanaotumia wanaojiita mawakala wa udahili wa vyuo vikuu, TCU imetaka wananchi kuchukua tahadhari.
“TCU inawaasa wananchi kuepuka kupotoshwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini,” imesema taarifa hiyo.