Rais Samia mgeni rasmi siku ya mashujaa

HomeKitaifa

Rais Samia mgeni rasmi siku ya mashujaa

AMIRI Jeshi Mkuu, Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa kitaifa Julai 25, mwaka huu.

Sherehe za kilele hicho zitakafanyika eneo jipya ulipojengwa Mnara wa Mashujaa katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Akizungumza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema viongozi wa mkoa huo wamekaribisha wananchi wote mkoani hapa na mikoa mingine jirani ya Singida, Iringa, Manyara na Morogoro katika siku ya maadhimisho hayo.

Awali, maadhimisho hayo yalikuwa yanafanyika katika Viwanja vya Jamatin katikati ya Jiji ambao ulikuwa mdogo na hivyo Rais Samia akatoa maelekezo kwamba utafutwe uwanja mwingine na ukatafutwa katika mji wa Serikali.

Amempongeza Rais Samia kwa kutoa fedha za kujenga na kukamilisha ujenzi wa mnara huo na hasa kusimamia agizo lake la kujenga mnara huo katika eneo kubwa.

Maadhimisho hayo yanafanyika kwa ajili ya kuwakumbuka mashujaa waliotetea, kupigania na waliopoteza uhai kwa ajili ya kupigania na kulinda uhuru wa nchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Kabla ya kilele cha maadhimisho hayo, kutakuwa na uwashaji wa Mwenge wa Mashujaa saa 6:00 usiku ya Julai 24 kuamkia Julai 25 na utaongozwa na Mkuu wa Mkoa Senyamule na mwenge huo utazimwa na Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe saa 6:00 usiku wa Julai 25 baada ya maadhimisho hayo.

Mkuu huyo wa mkoa aliwaomba wananchi kutumia maadhimisho hayo katika kudumisha na kuimarisha umoja wa kitaifa, amani na utulivu ili kutumia muda mwingi katika kubuni na kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo.

error: Content is protected !!