Hakuna uhaba wa mafuta nchini

HomeKitaifa

Hakuna uhaba wa mafuta nchini

WAKALA wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) umesema hakuna uhaba wa mafuta nchini.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa PBPA, Erasto Mulokozi amelieleza HabariLEO kuwa mafuta yaliyopo kwenye maghala na yanayoshushwa bandarini yanatosheleza mahitaji ya mafuta nchini.

Mulokozi alisema Dar es Salaam jana kuwa wao wana akiba ya kutosha ila tatizo linaweza kuwa kwa wasambazaji inayojumuisha vituo vya mafuta.

“Kuna meli inaendelea kushusha mafuta aina ya petroli toka juzi na tunatarajia itamaliza kushusha kesho au keshokutwa hii ilikuwa na lita karibia milioni 55,” ameeleza Mulokozi.

Ameongeza: “Halafu kuna meli ya dizeli ambayo imefunga jana inatarajia kuanza kushusha baada ya hii kumaliza ina lita karibia 150, pia kuna meli ya petroli tena imefika jana inasubiri hizo mbili ziondoke nayo ianze kushusha yenye lita milioni 155.”

Mulokozi amesema akiba ya mafuta na upatikanaji wake PBPA bado ipo salama, lakini inawezekana mtandao wa usambazaji kwenda kwa mtumiaji wa mwisho una shida.

“Kuna changamoto kwenye usambazaji, sisi kwenye upatikanaji wa bidhaa ya mafuta tupo sawa, ila kwenye mtandao wa usambazaji ndio kuna shida si unaona kuna watu wanayaficha kule ndio kwenye changamoto huku juu hakuna shida,” amesema.

Mulokozi amesema wafanyabiashara wanaodaiwa kuficha mafuta, mamlaka ya kuwaadhibu ipo kwenye Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Amekemea tabia ya wanaoeneza taarifa za uongo kuwa kuna uhaba wa mafuta nchini kwa kuwa zinaleta taharuki kwa watumiaji wa nishati hiyo.

Mwanzoni mwa wiki hii, Ewura ilizionya kampuni za mafuta zinazohodhi mafuta ya petroli kwa maslahi binafsi.

Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Mwainyekule ilizitaka kampuni hizo ziache kuhodhi mafuta kwa kuwa ni kinyume cha sheria, kanuni zinazosimamia biashara ya mafuta ya petroli nchini na masharti ya leseni za biashara zao.

Mwainyekule alieleza kuwa Ewura imepata taarifa kuna kampuni za mafuta zinazohodhi bidhaa hiyo kwa ajili ya maslahi ya kibiashara ikiwa ni pamoja na kusubiri mabadiliko ya bei.

error: Content is protected !!