Tanzania na Ujerumani zinatarajia kuanza mazungumzo rasmi juu ya yaliyojiri wakati wa ukoloni ikiwemo kurejesha mabaki ya miili na mafuvu yaliyochukuliwa kipindi hicho.
Mazungumzo hayo ni miongoni mwa masuala muhimu ya kihistoria yaliyoangaziwa katika maongezi ya Rais Samia na Rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier, ambaye yupo nchini katika ziara ya siku tatu iliyoanza Oktoba 30 mwaka huu.
Rais Samia amewaambia wanahabari Ikulu jijini Dar es Salaam jana Oktoba 31, 2023 kuwa mazungumzo baina ya nchi hizo mbili yatatoa mwongozo utakaowezesha baadhi ya watanzania kupata mabaki ya miili ya ndugu zao yaliyopo nchini Ujerumani.
“Tumezungumza kwa urefu na tupo tayari kufungua majadiliano na kuona jinisi tutakavyoweza kukubaliana kwa yale yaliyopita wakati wa utawala wa Ujerumani hapa nchini kwetu au ndani ya taifa letu,” alisema Rais Samia.
Ujerumani iliitawala Tanzania Bara wakati huo ikiitwa Tanganyika mnamo mwaka 1885 mpaka mwaka 1918 wakati wa vita ya kwanza ya dunia na kuiachia nchi ya uingereza iliyotawala mpaka wakati wa uhuru.
Katika utawala wake Ujerumani ilichukua baadhi ya vito vya thamani, mabaki ya maliasili za kihistoria na mafuvu ya watu mashuhuri waliopigana vita dhidi yake yaliyozipamba makumbusho ya Ujerumani.
Ujerumani ilifanya hivyo pia katika baadhi ya makoloni yake barani Afrika yaikiwemo Rwanda na Burundi.
“Kuna familia ambazo zinasubiri mabaki ya wapendwa wao ambao wapo kule katika makumbusho mbalimbali za Ujerumani yote hayo tunakwenda kuzungumza na kuona vipi twende nayo vizuri,” alisema Rais Samia.
Mapema Mwezi Januari mwaka huu Mamlaka ya Makumbusho ya Berlin ilisema ipo tayari kurudisha baadhi ya mafuvu yaliyochukuliwa katika makoloni yake yaliyopita.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ujerumani (DW) wanasayansi walichunguza jumla ya mafuvu 1,135 na kubaini mafuvu 904 yanaweza kuwa yalitokea Rwanda, 202 kutoka Tanzania na 22 ni ya Kenya.
Rais Steinmeier, amesema pamoja na mambo mengine atatumia ziara yake nchini Tanzania kukusanya maoni yatakayowezesha urejeshwaji wa mabaki ya miili ambayo bado yapo nchini mwao.