Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara linawashikilia walimu sita wa shule ya Sekondari Makongoro, wilayani Bunda, kuhusiana na kifo cha mwanafunzi wa kidato cha sita, Peter Marire (23), kinachodaiwa kutokea baada ya kupewa adhabu ya kuchapwa kwa madai ya kufanya vibaya katika mtihani wa majaribio.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, amesema uchunguzi unaendelea kwa ushirikiano kati ya polisi na wataalamu wa afya ili kubaini chanzo halisi na mazingira ya kifo hicho.
Amesema baada ya tukio hilo, askari walipelekwa shuleni kuimarisha usalama kufuatia taharuki miongoni mwa wanafunzi waliotishia kufanya vurugu.
Kamanda Lutumo amewataka wananchi na wanafunzi kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea, akisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kulingana na matokeo ya uchunguzi.


