Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia Hussein Idd (37), mlinzi na mkazi wa Kayenzi, Manispaa ya Morogoro, kwa tuhuma za kumuua kwa risasi Feisal Yaqoob (43), dereva wa lori aina ya Scania na mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam.
Polisi wamesema tukio hilo limetokea leo majira ya saa 12:00 alfajiri katika kituo cha mafuta kilichopo Mtaa wa Viwandani, Kata ya Kihonda, ambapo marehemu alikuwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea Mwanza na alikuwa ameegesha lori lake katika kituo hicho kabla ya kwenda kuswali katika msikiti wa eneo hilo.
Baada ya kurejea, mtuhumiwa alimtaka alipe TZS 15,000 kama malipo ya ulinzi wa lori hilo. Inadaiwa dereva alikataa kutoa fedha hizo na kuanza kuondoka, ndipo mlinzi huyo alipomfyatulia risasi kichwani, na kusababisha kifo chake papo hapo.


