Leo Rais Samia Suluhu, alikuwa jijini Mwanza akihitimisha tamasha la utamaduni. Moja kati ya mambo makubwa yaliyofanyika katika tamasha hilo, ni umoja wa machifu wa Kisukuma kwa niaba ya umoja wa Machifu wa Tanzania kumtawaza Rais Samia Suluhu kuwa mkuu wa machifu wote wa Tanzania.
Rais Samia alieleza kwamba tendo hili lina maana kubwa katika utamaduni wa Kitanzania, likimaanisha kwamba sasa amepata baraka rasmi kwa mujibu wa tamaduni zetu.
Aidha machifu hao walimpa Rais Samia jina linaloendana na uongozi wake kama chifu wa Tanzania yote. Jina hilo ni ‘Hangaya’ likiwa linamaanisha nyota ang’avu.
Katibu wa Umoja wa machifu wa Kisukuma, Mtemi Aaroni Mikomangwa amesema jina hilo ni kutambua mchango wa Serikali anayoiongoza kwa kuthamini na kusimamia utu wa wanyonge pamoja na utamaduni wa Mtanzania.
“Unathamini kazi, ushirikiano, upendo na utu, tunaishukuru Serikali yako kwa kuthamini na kuenzi michango yetu Watanzania wote ikiwepo kuboresha sera za utamaduni kwa kushirikisha asasi za jadi nasi tu pamoja nawe katika kuinua utamaduni wa Taifa letu,” alisema Mtemi Mikomangwa.