Wabunge wa Umoja wa Ulaya waridhishwa na mwelekeo wa kiuchumi na kisiasa nchini Tanzania

HomeKitaifa

Wabunge wa Umoja wa Ulaya waridhishwa na mwelekeo wa kiuchumi na kisiasa nchini Tanzania

Baadhi ya wajumbe wa Bunge la Umoja wa Ulaya wameelezea kuridhishwa kwao na mwelekeo wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan tangu kuingia kwake madarakani mwezi Machi mwaka huu na kumpa pongezi kwa kazi yake kubwa aliyoifanya ndani ya miezi michache huku wakiahidi kushirikiana zaidi na Tanzania.

Wakizungumza mapema leo, mmoja wa Wabunge hao Bi Rita Laranjinha ameeleza kwamba, Rais Samia ameonyesha mwanzo mzuri tangu kuingia kwake madarakani kwa kuweza kufanya vizuri kitaifa na kimataifa huku wakitaja baadhi ya mambo makubwa na yenye faida kwa Tanzania aliyoyafanya ndani ya muda mchache.

Moja wametoa pongezi kwa Rais Samia kuongoza Tanzania katika kipindi cha mpito bila machafuko baada ya kifo cha Rais Dkt John Pombe Magufuli. Pongezi hizi zinatokana na hulka ya mataifa mengi Afrika kutofuata mwongozo wa Katiba na kuingia katika machafuko ya kugombea madaraka wakati Rais aliye madarakani anapofariki.

Pili, Wabunge hao wametoa pongezi kwa Rais kuheshimu uhuru wa kujieleza na ule wa vyombo vya habari. Tangu kuingia kwake Rais Samia Suluhu Hassan madarakani vyombo vya habari vimekuwa huru kufanya kazi zake bila woga, vikitoa taarifa kwa wananchi kama ilivyotakiwa.

Tatu, pongezi imekwenda katika eneo la usawa wa kijinsia hasa ushirikishaji wa wanawake katika nafasi za juu za uongozi, mfano Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ,Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Nchi. Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa na Waziri wa Ulinzi mwanamke Tangu kupata uhuru.

Nne, Umoja huo umetoa pongezi kwa Rais Samia kuelewa na kuunga mkono chanjo ya Uviko-19 jambo ambalo pia limefungua sekta ya utalii nchini kwa kiasi kikubwa mpaka sasa baada ya mdororo wa sekta hiyo uliotokana na kuenea kwa homa ya korona.

Tano, katika sehemu ya pongezi zake umoja huo umeeleza kuridhishwa kwake na hatua ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kubadili mfumo na kuruhusu wanafunzi waliopata mimba au kukatisha masomo kwa sababu mbalimbali kurejea shuleni. Mbali na haki ya elimu hatua hii inalenga kuwapa nafasi waliokosa elimu kuipata ili kujikwamua kimaisha kwa maarifa na ujuzi.

Katika hitimisho lao wabunge hao wameeleza kuendelea kuwa na matumaini ya kuona mabadiliko chanya zaidi nchini baada ya kuona mengi mazuri katika kipindi cha muda mfupi wa uongozi wa Rais Samia. Mwisho kabisa Umoja wa Ulaya umesema kwamba Tanzania itabaki kuwa mshiriki muhimu wa Umoja huo na kuahidi kushirikiana katika nyanja mbalimbali za kimataifa, kitaifa, biashara na uchumi pia katika suala zima la kulinda haki za binadamu.

error: Content is protected !!