Huenda maadhimisho ya Nane Nane ya mwaka huu yatawapatia wakulima matumaini mapya katika msimu mpya wa kilimo baada ya Serikali kuzindua mpango wa ruzuku kwa pembejeo.
Hatua hiyo itapunguzia wakulima waliokuwa wakitumia awali kupata pembejeo za kilimo, jambo linaloweza kuongeza uzalishaji na masoko ya kilimo.
Akizungungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika mkoani Mbeya jana Agosti 8 wakati wa kilele cha sherehe za Wakulima Nane Nane, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema mpango huo unalenga kuwaondolea mzigo wakulima kutokana na changamoto za bei za mbolea.
Amesema kupitia mpango huo mbolea zote za kupandia zinazofahamika kama NPK zilizokuwa zikiuzwa kwa Sh122, 695 zitauzwa kwa Sh70 000 huku ruzuku ya Serikali ikiwa Sh52,695.
“UREA (ya kukuzia) itatoka Sh124,734 wakulima wataenda kuinunua kwa Sh70,000,” amesema Bashe.
Ili kunufaika na mpango huo wakulima wanatakiwa kuandikishwa na kuhakikisha wananunua pembejeo hizo kwa bei elekezi.
Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akihutubia kwenye kilele cha maadhimisho ya Nanenane ambayo yamefanyika kitaifa katika Viwanja vya John Mwakangale jijini humo, ameagiza mpango huo wa ruzuku ya pembejeo kuanza Agosti 15 ili kuwawezesha wakulima kujipanga na msimu mpya wa kilimo.
‘’Waziri wa fedha umeniambia fedha ziko tayari ila kuna taratibu zinatakiwa zitimie, lakini nataka niseme kwamba ruzuku hizi zianze kuanzia Agosti 15 ili wakulima wajitayarishe kuanza msimu unaokuja,” amesema Rais Samia.
Rais Samia atoa maagizo
Katika maadhimisho hayo Rais Samia ametaka kila mkoa kuhakikisha wanatenga eneo kwa ajili ya kilimo cha mashamba makubwa pamoja na kujikita kwenye kilimo cha biashara ili kukuza uchumi wa nchi.
“Kila mkoa upange eneo kubwa kwa lile zao ambao kwa mkoa ule litamea vizuri na kuzalishwa jwa tija, “amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amesema Serikali imejipanga kuwawezesha vijana kujiingiza kwenye kilimo ambapo watapewa hati na kuunganishwa kwenye mikopo rahisi isiyo na riba kubwa.
“Niwaombe vijana ingieni kwenye shughuli hii ya kilimo,” amesema Rais.