Bodi na Menejimenti ya TASAC yafanya ziara mkoani Mtwara

HomeKitaifa

Bodi na Menejimenti ya TASAC yafanya ziara mkoani Mtwara

Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi Nahodha. Mussa Mandia imefanya ziara mkoani Mtwara tarehe 06 Novemba, 2023 ikiwa na lengo la kutembelea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Shirika hilo ikiwa ni pamoja na kuwatembelea watoa huduma wanaodhibitiwa na TASAC.

Wajumbe wa Bodi hiyo na Menejimenti wamepata fursa ya kutembelea meli za kigeni zinazokuja Mkoani Mtwara na kupata taarifa ya vyombo vidogo vinavyokaguliwa na TASAC katika mialo mbalimbali katika ukanda huo.

Pia, Bodi imetembelea maeneo binafsi yanayojihusisha na utoaji huduma za usafirishaji kwa njia ya maji kwa maana ya watoa huduma wa upakiaji wa Korosho na kuzileta bandarini kwa wale waliopewa vibali maalumu au leseni na Shirika ili kusaidia bandari katika kuwezesha shughuli zake.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo Capt. Mussa Mandia akizungumza na waandishi wa habari katika ziara hiyo ya kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na TASAC chini ya usimamizi wa Bodi hiyo.

Aidha, Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya TASAC wamepata fursa ya kujionea utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kupakia shehena ya korosho kupitia bandari ya Mtwara kwenda nchi za nje, hilo limeendelea kufanyika na kujionea shughuli hiyo ikifanyika kwa ufasaha na ufanisi kwa kutenga upakiaji wa makaa ya mawe na upakiaji wa korosho na hakuna muingiliano wa aina yoyote katika upakiaji wa bidhaa hizi.

Ziara hii imekamilishwa kwa kuangalia ufanisi na uwekezaji wa serikali kupitia TPA kwa lengo la kuchochea na kukuza uchumi wa Mkoa huu na kuleta maendeleo kwa Taifa.

Ziara hiyo imeanza tarehe 06 Novemba, 2023 na inatarajiwa kuhitimishwa tarehe 11 Novemba, 2023.

Aidha, Bodi imeunga mkono na kupongeza jitihada za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kujenga bandari ya kuhudumia mizigo mchafu eneo la Kisiwa-Mgao, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Mkoani hapo.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Capt. Mussa Mandia akiwa katika ziara hiyo ya kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na TASAC chini ya usimamizi wa Bodi hiyo.

error: Content is protected !!