Timu ya Taifa ya Brazil ambayo ndio timu inayoongozwa kwa ubora wa soka duniani kwa mujibu wa viwango vya Shirikisho la mpira duniani (FIFA), imeshindwa kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali baada ya kuondoshwa na timu ya Taifa ya Croatia kwa changamoto ya mikwaju ya penati.
Katika mchezo huo wa hatua ya robo fainali, Brazil ndio ilikua ya kwanza kujipatia goli kupitia kwa mchezaji wake Neymar huku katika dakika 105+1, Croatia likifungwa naye Bruno Petkovic dakika ya 117 yote yakifungwa katika muda ule wa nyongeza wa dakika 30 baada ya dakika 90 kuisha kwa sare ya bila kufungana na kupelekea mchezo huo kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti ambapo Croatia walifanikiwa kuibuka wababe kwa kufunga penati nne dhidi ya mbili za Brazil ambao walikosa penalti mbili zilizopigwa na Rodrygo pamoja na Marquinhos.
Katika mchezo mwingine wa hatua hiyo ya robo fainali mahasimu wa jadi wa Brazil timu ya taifa ya Argentina ilifanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kuishinda timu ya taifa ya Netherland (Uholanzi) kwa changamoto ya mikwaju ya penati pia.
Brazil inayaaga mashindano hayo ikiwa bado ndio timu inayongoza kwa kutwaa Kombe la Dunia mara tano. Brazil ilitwaa taji hilo nchini Sweden mwaka 1958, nchini Chile (1962), Mexico (1970), Marekani (1994) na Korea/Japan (2002), tangu mwaka 2002 Brazil haikuweza kufanya vizuri tena katika mashindano hayo makubwa ya soka duniani.