Daraja la Tanzanite kubadilishwa

HomeKitaifa

Daraja la Tanzanite kubadilishwa

Rais Samia Suluhu Hassan amezindua daraja la jipya la Selander maarufu kama Tanzanite la jijini Dar es Salaam huku akipendekeza alama ya mwenge iliyoweka juu ya daraja hilo ibadilishwe na iwekwe alama ya madini ya Tanzania ili kusadifu jina la daraja hilo.

Daraja hilo ambalo lilianza kutumiwa Februari 1 mwaka huu liliwekewa alama ya Mwenge wa Uhuru katika moja ya nguzo zake ili kutambua tunu hiyo muhimu katika maendeleo ya Tanzania.

Hata hivyo, Rais Samia aliyekuwa akizindua daraja hilo leo Machi 23, 2022 amesema amepokea mapendekezo kutoka kwa wananchi kuhusu alama ya mwenge iliyowekwa juu ya daraja hilo na anaona kuna umuhimu ibadilishwe.

“Ushauri niliopata kwa wananchi daraja hili tunaliita la  daraja la Tanzanite lakini alama tuliyoiweka ni alama ya Mwenge (wa Uhuru).  Pamoja na kutambua mwenge ni tunu yetu adhimu, wananchi wangependa sana kuona umbo la Tanzanite pale ulipo Mwenge ili kukamilisha jina la daraja hili,” amesema Rais Samia.

Aidha, kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema daraja hilo ni muendelezo wa uboreshaji wa miundombinu ya usafiri jijini humo ili kuchagiza shughuli za uzalishaji na biashara kufanyika bila vikwazo.

“Tukipunguza muda wa watu kukaa barabarani maana yake tunaongeza muda wa watu kufanya kazi. Lakini pia kupunguza gharam za mafuta yanayotumiwa na vyombo vya usafiri. Nadhani tutapunguza migogoro majumbani kwa watu kuchelewa kwa kusingizia foleni,” amesema  Rais Samia.

Kwa mujibu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TBA), Daraja hilo linalokatiza katika Bahari ya Hindi kwa kuunganisha barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Barack Obama lina urefu wa kilomita 1.30 na barabara unganishi kilomita 5.2 ambapo limegharimu Sh243 bilioni hadi kukamila kwake.

Daraja la Tanzanite ni mojawapo ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya kupunguza msongamano wa magari yanayoingia na kutoka katika jiji la Dar es Salaam.

Ujenzi wa daraja hilo ulianza mwaka 2018, ambapo kazi ya usanifu ilikuwa imekamilika na kazi zilianza kwa kuchimba msingi ambapo nguzo zaidi ya 200 zimeingia chini ya bahari.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema daraja hilo litapunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam  kwa sababu kwa sasa linapitisha magari kati ya 17,726 hadi 19,764 Jumatatu hadi Ijumaa.

Amesema pia litakuwa kivutio cha utalii na kupunguza ajali za barabarani kwa sababu lina sehemu ya watembea kwa miguu huku likichochea shughuli za kiuchumi na kibiashara jijini humo.

error: Content is protected !!