Fahamu mapendekezo ya Kikosi Kazi kuhusu Katiba Mpya

HomeKitaifa

Fahamu mapendekezo ya Kikosi Kazi kuhusu Katiba Mpya

Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa nchini Tanzania kimesema mchakato wa kupata Katiba mpya uendelee kwa kupendekeza hatua sita zitakazorahisisha mchakato huo.

Mapendekezo hayo ni matokeo ya  uchambuzi wa mitizamo mitano tofauti  ya Watanzania kuhusu Katiba mpya ambapo baadhi walipendekeza kuanza mchakato kuanza upya, huku wengine wakishauri iliyopo iboreshwe.

Profesa Rwekaza Mukandala ambaye ni mwenyekiti wa kikosi kazi hicho ametoa mapendekezo hayo alipokuwa akiwasilisha ripoti iliyoundwa na kikosi kazi kwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 21, 2022.

Mkandala amependekeza kuwa kwanza ufanyike mjadala wa kitaifa kuhusu masuala ya msingi ili upatikane muafaka kabla ya kuanza kuandika Katiba mpya.“Mjadala huu ufanyike kwa ushiriki mpana wa wananchi, masuala ya msingi yatakayojadiliwa ni pamoja na muundo wa muungano, madaraka ya Rais mfumo wa uchaguzi, madaraka ya serikali za mitaa, maadili, rushwa pamoja na masuala mengine yatakayoibuka,” amesema Prof Mkandala.

Hatua ya pili iliyopendekezwa ni kuhuisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria ya Kura ya Maoni ili kuweka mahitaji ya sasa ikiwemo kuainisha muda wa mchakato mzima, kutambua jopo la wataalamu pamoja na misingi ya kuzingatia.

Mkandala amesema baada ya  Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Rais wa Tanzania kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wataunda jopo la wataalam litakalopitia mapendekezo yaliyotolewa na kuandaa rasimu mpya.

“Jopo la wataalamu linatakiwa kuzingatia, kufanya mapitio ya Katiba inayopendekezwa ya mwaka 2014 kwa kuzingatia hali ya sasa kiuchumi, kisiasa na kijamii,” amesema MUkandala ikiwa ni sehemu ya mapendekezo ya kikosi kazi.

Aidha jopo hilo litakaloundwa litatakiwa kurejea baadhi ya nyaraka ikiwemo Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, rasimu ya pili ya Tume ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 pamoja na ripoti ya Serikali kuhusu masuala muhimu ya kitaifa katika mjadala wa kitaifa.

Mara baada ya jopo hio kuandaa rasimu, kikosi kazi kinapedekeza ripoti kuwasilishwa kwa Bunge la Tanzania kwa ajili ya kujadiliwa pamoja na kupitishwa kuwa Katiba inayopendekezwa ambapo majukumu ya bunge yataaainishwa katika  Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Kikosi kazi kimeshauri wananchi kupewa elimu ya uraia kuhusu Katiba inayopendekezwa  kabla ya kupiga kura ili waifahamu na kuwaandaa kufanya maamuzi sahihi.

 

error: Content is protected !!