Fahamu tabia 5 zinazoshusha thamani ya vijana mahali pa kazi

HomeElimu

Fahamu tabia 5 zinazoshusha thamani ya vijana mahali pa kazi

Baadhi ya vijana wametokea familia duni lakini wakafanikiwa zaidi maishani kuliko waliotoka familia zenye ukwasi. Vivyo hivyo, wapo waliotoka katika familia za kitajiri wamefanikiwa kwa yale wanayofanya katika kazi zao kuliko hata waliotoka kwenye maisha duni.

Utofauti huo wa mafanikio katika kazi zetu au taaluma zetu ni matokeo ya mambo katika maisha kuanzia malezi katika familia zetu, mfumo wa jamii na tabia binafsi za vijana.Licha ya kuwepo sababu lukuki katika hili, kuna tabia mashuhuri ambazo hufanya vijana wengi kupoteza mwelekeo katika kazi zao hususan mahala pa kazi.

  1. Dharau
    Dharau huvunja ushirikiano kazini na hutengeneza maadui. Matokeo ya dharau ni kiburi ambacho ni kaburi la kitaaluma na kimaisha kwa vijana wengi sana. Huwezi kupandishwa cheo kuwa kiongozi kama unadharau. Huwezi kuwa na wateja wengi au washirika wengi wa kibiashara kama unadharau. Dharau inaua ndoto.
  2. Kutojiongeza kitaaluma
    Vijana wengi wa namna hii licha ya kuwa damu bado inachemka, huwa wa kwanza kuondolewa kazini kwa kuwa hawaongezi thamani yeyote katika taasisi pale inapotokea kuna upunguzaji wa wafanyakazi. Ili kudumu na kukua vyema kitaaluma, ni vema vijana wakajiongeza kimaarifa kwa kutafuta mafunzo ya mtandaoni ya bure ama ya kuyalipia kidogo. Jitihada za namna hii huziba mwanya wa maarifa hasa pale mashirika wanayofanyia kazi yanaposhindwa kugharamia mafunzo.

    > Mambo matano ya kuzingatia kwenye barua ya kuomba kazi

  3. Uvivu
    Ili kutokomeza tabia hii, vijana tunatakiwa kujipangia malengo binafsi yanayolandana na kazi zetu ili kuhakikisha tunayafanikisha. Weka mpango wa kuwahi mapema mahali pa kazi, fanya kazi kwa wakati na jenga mazoea ya kuhakiki maendeleo yako kila siku.
  4. Utovu wa nidhamu
    Kijana smati ni yule mwenye nidhamu ya kazi na maisha yake. Nidhamu hufanya kijana makini kuheshimu na kuheshimu wengine bila kujali uwezo au hali zao za kielimu. Kwa kifupi mtu wa namna hii huwa ni “konki wa mafanikio”. Vijana wengi waliofanikiwa wakiwemo mabilionea kama Mark Zukerberg wa Facebook huwezi kukuta wakiwa na skendo nyingi za utovu wa nidhamu ukiachana na changamoto za kampuni wanazoziongoza.
  5. Kupoteza muda
    Kuchati kwenye mitandao ya kijamii kama makundi ya Whatsapp au kupiga umbea wakati wa kazi ni moja ya masuala ambayo kwa sasa yanawapotezea muda vijana. Tabia hii imekuwa ikiwafanya washindwe kutimiza malengo yao ya kikazi au kibiashara na kuhatarisha vibarua au biashara zao.

Hivyo basi kama kijana mwenye nia yakufikia malengo ni vyema ukaacha tabia hizo iliuweze kukamilisha ndoto zako.

error: Content is protected !!