January Makamba aanza na TANESCO

HomeKitaifa

January Makamba aanza na TANESCO

Waziri wa wa Nishati, January Makamba (MB) amefanya ziara fupi kwenye kituo cha udhibiti wa mfumo wa usafirishaji umeme (GCC) kilichopo  Ubungo jijini Dar es Salaam, ikiwa ni shughuli yake ya kwanza nje ya ofisi tangu awe Waziri wa Nishati.

Makamba ameeleza kuwa amefanya ziara hiyo kufuatia malalamiko ya mengi ya wananchi, kuhusu kukatika kwa umeme mara kwa mara ambako kumekuwa kujitokeza hivi karibuni. Kwa mujibu wa Waziri Makamba, TANESCO wametoa sababu mbalimbali zilizosababisha kadhia hiyo lakini yeye amebaini mambo manne yanayosababisha hali hiyo.

Mambo hayo ni pamoja na kukosa mfumo wa kiteknolojia wa kubaini kwa haraka ukatikaji wa umeme kwenye maeneno mengi mtaani, wananchi kutopewa taarifa za awali kuhusu kuzimwa kwa umeme kutokana na matengenezo yaliyopangwa, wananchi kukosa namna ya uhakika ya kutoa taarifa kuhusu kukatika kwa umeme na changamoto nyinginezo, na mwisho matengenezo ya kawaida ya miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme kutofanyika kwa kiwango stahiki.

Kufuatia hayo, Waziri Makamba ameielekza TANESCO kuchukua hatua za haraka, ikiwa ni  pamoja na kuhakikisha tatizo la kukatika kwa umeme hasa pale linapotokana na uzembe na ucheleweshaji wa matengenezo linaisha ndani ya wiki mbili.  Amesema zaidi ya hapo, watalazimika kuwaondoa kazini wahusika.

Aidha, Makamba ameielekeza TANESCO  kuimarisha mfumo wa huduma kwa wateja, na pia viongozi na wawakilishi wa shirika wajitokeze kwenye vipindi vya moja kwa moja katika vyombo vya habari na kupokea kero za wateja kuhusu huduma ya umeme na kuzitolea majawabu.

Pia TANESCO imetakiwa kuhakikisha kwamba matengenezo na maboresho yanayopaswa kufanywa kwenye mfumo wa usafirishaji na usambazaji yanafanyika bila kuchelewa.

Waziri Mkamba pia ametanabaisha kwamba, mabadiliko makubwa yanakuja ndani ya TANESCO.

error: Content is protected !!