Jinsi kampuni za simu Tanzania zinavyoweza kutoa taarifa za siri za wateja wao

HomeBiashara

Jinsi kampuni za simu Tanzania zinavyoweza kutoa taarifa za siri za wateja wao

Mtumiaji wa huduma za mawasaliano ana haki mbalimbali zinazopaswa kulindwa na mtoa huduma za mawasiliano.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeanisha haki za mtumiaji wa huduma za mawasiliano ikiwemo zile zinazotolewa na kampuni za simu.

Haki hizo ni pamoja na kupata huduma bora, kupewa taarifa kuhusu huduma au bidhaa, kutobaguliwa, kulalamika na kutatuliwa malalamiko yake, kuhakikishiwa usalama wa bidhaa au huduma.

Nyingine ni kuwa na faragha na usiri katika matumizi yake, kuelimishwa, kupewa taarifa kabla ya kusimamishwa au kukatisha huduma, kuwakilishwa, kupewa taarifa sahihi ya ankara na kukata rufaa endapo haridhishwi na matumizi.

Haki zote hizo hulindwa kwa mujibu wa Sheria mbalimbali zikiwemo Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ya mwaka 2003, Sheria ya Mawasilianp ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010 na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya mwaka 2015.

Haki ya usiri na faragha katika matumizi ni kati ya haki zinazojadiliwa zaidi na wengi kwani watu wengi wasingependa taarifa zao zijulikane na wale wasiohusika.

Sheria inawataka watoa huduma kulinda taarifa za wateja na kutozitoa bila idhini ya wahusika ambayo inapaswa kutolewa kwa maandishi.

Hata hivyo, watoa huduma za mawasiliano ambao ni pamoja na kampuni za simu wanatakiwa kutoa taarifa za mteja wao iwapo wataelekezwa kufanya hivyo na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) ili zikatumike katika uchunguzi wa matukio ya kijinai ama itakapoombwa na Mahakama.

Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010 ni kati ya Sheria zinzoeleza masuala yahusuyo utaratibu wa kulinda faragha, hususan katika vifungu vya 98 na 99.

Hivyo fahamu, yapo mazingira ya kisheria yanayoweza kufanya kampuni ya simu itoe taarifa za mteja wao.

error: Content is protected !!