Kushuka kwa bei za vyakula

HomeBiashara

Kushuka kwa bei za vyakula

Huenda maumivu ya kupanda kwa bidhaa Tanzania yakapungua siku za hivi karibuni baada ya wataalam wa uchumi kueleza kuwa bei za vyakula duniani zilishuka mwezi ulipita na zinaweza kuendelea kushuka zaidi. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) katika ripoti yake ya hali ya bei ya vyakula duniani iliyotolewa mjini Roma, Italia Aprili 6, 2022, limesema bei za bidhaa za chakula duniani zilipungua mwezi Aprili mwaka huu baada ya kupanda kwa kiwango kikubwa mwezi Machi.

Ushukaji huu umetajwa kuongozwa na kushuka kidogo kwa bei ya mafuta ya mboga na nafaka, huku bei ya mchele, nyama, maziwa na sukari ikiongezeka kidogo na matarajio ya biashara ya kimataifa yakififia.

“Kupungua kidogo kwa bei ni afueni inayokaribishwa, hasa kwa nchi za kipato cha chini zenye upungufu wa chakula, lakini bado bei za vyakula zinasalia kuwa karibu na viwango vya juu vya hivi karibuni, jambo linaloakisi mkwamo wa soko na kuleta changamoto kwa uhakika wa chakula duniani kwa walio hatarini zaidi,” Mchumi Mkuu wa FAO, Máximo Torero Cullen amesema.

Kwa mujibu wa FAO vita ya Ukraine imeendelea kuwa na athari kwa namna moja ama nyingine duniani kwenye sekta ya chakula hususan vyakula vinavyotoka bara la Ulaya.

Miongoni mwa bei ambazo zimeongeka kwa mwezi Aprili zilizoripotiwa na FAO ni pamoja na sukari ambapo ilirekodiwa ongezeko la asilimia 3.3 sababu ikielezwa ni mavuno kidogo kutoka kwa msambazaji mkubwa duniani nchi ya Brazil.

Pia nyama nayo iliongezeka bei kwa asilimia 2.2 na kuweka rekodi mpya ya juu huku bei za kuku na nyama ya ng’ombe zikielezwa kuathiriwa na vita ya Ukraine pamoja na milipuko ya mafua ya ndege.

Bei ya maziwa nayo iliongezeka kwa asilimia 0.9 kutokana na kubanwa kwa ugavi duniani huku uzalishaji wa maziwa huko Ulaya Magharibi na maeneo mengine ukiendelea kuwa wa kiwango cha chini.

FAO imetoa muhtasari mpya wa ugavi wa nafaka na mahitaji yenye utabiri unaoashiria uwezekano wa kupungua kwa asilimia 1.2 katika biashara ya kimataifa ya nafaka katika mwaka wa masoko wa 2021/22 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Kupungua huko kunahusishwa na mahindi na nafaka nyingine huku kiasi cha biashara ya mchele kikitabiriwa kukua kwa asilimia 3.8 na kile cha ngano kwa asilimia 1.

FAO imeendelea kutabiri uzalishaji wa ngano duniani kukua mwaka 2022, hadi tani milioni 782. Utabiri huo unajumuisha kupungua kwa asilimia 20 ya uzalishaji kwa eneo lililovunwa nchini Ukraine pamoja na kupungua kwa mazao yanayotokana na ukame nchini Morocco.

 

SOURCE: NUKTA HABARI

 

error: Content is protected !!