Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema Rais Samia Suluhu ameielekeza wizara hiyi kuhakikisha ujenzi wa mradi wa bomba la gesi kutoka Tanzania hadi Uganda upitie katika makazi ya watu ili kurahisisha ufikaji wa nishati hiyo katika maeneo ya vijijini.
“Rais ameelekeza ujenzi wake upitie katika makazi ya watu ili wanufaike na gesi kama wanavyofaidika wakazi wa Dar es Salaam na sio kulipitisha katika mtaro wa bomba la mafuta kutoka Uganda,” alisema Mramba.
Mramba alisema lengo la Rais Samia ni kuona nishati ya gesi inaendelea kusambazwa katika maeneo mbalimbali ili Watanzania wote wanufaike na kuinua kipato chao na taifa kwa ujumla.
Alieleza kuwa serikali ipo katika hatua za mwisho kuanza kusafirisha gesi mikoani ikianza na Mkoa wa Dodoma ambako itajengwa bohari kubwa ya gesi itakayojazwa kwa kutumia malori.
Pia alisema, Rais Samia ameidhinisha Sh bilioni 500 kwa ajili ya kuboresha mifumo ya umeme ili kukatika ovyo na kurekebisha maeneo ambayo mfumo umeelemewa kwa kuanzisha mfumo mwingine.