Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makalla amekutana na uongozi wa wafanyabiashara wadogo wadogo (Machinga) wa mkoa huo ili kutafuta njia bora ya kuwapanga kuondoa usumbufu.
Akizungumza katika kikao hicho, Makalla ameeleza kufurahi kwake kuona kikao hicho kimemalizika kwa mafanikio makubwa ambapo ameahidi kushughulikia mapendekezo yote yaliyotolewa kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya wa mkoa huo.
Amesema miongoni mwa maeneo atakayoanza kuyafanyia kazi ni pamoja na kuwapanga Machinga waliojenga vibanda juu ya mitaro na mifereji, wanaofanya biashara kwenye njia za watembea kwa miguu, wanaofanya biashara mbele ya maduka, wanaofanya biashara kwenye hifadhi ya barabara na wanaofanyabiashara mbele ya taasisi za umma zikiwemo shule kwenye mkoa huo.
Aidha alitumia fursa hiyo kwa viongozi wa wafanyabiashara hao kupendekeza maeneo ya wazi wanayoyaona yanafaa kwa biashara ili wapatiwe na ameahidi kuweka mazingira bora ya biashara ikiwemo kufikisha huduma ya usafiri.
Ameeleza kuwa serikali itaendelea kutoa elimu ya kutosha wafanyabiashara kwa kuwa lengo la serikali ni kuona biashara zinafanyika na watu wanapata kipato, na kwamba zoezi la kuwapanga litakuwa shirikishi.