Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amehudhuria na kushiriki Maadhimisho ya Miaka 10 ya Muungano wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) katika Ukumbi wa PSSSF jijini Dar es Salaam leo tarehe 13 Mei, 2022.
Katika maadhimisho hayo Rais Samia alizungumza mambo kadhaa kuhusu uanaharakati, utetezi wa haki za binadamu pamoja na ushirikiano baina ya serikali na wanaharakati/watetezi wa haki za binadamu.
Uanaharakati
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wanasiasa na watetezi wa haki za binadamu kuacha mapambano hasi na kufanya siasa chanya kwa masilahi ya taifa na sio kupambana na serikali.
“Siwakatazi kuwa wanaharakati, unaharakati chanya ndio unaojenga. Sisi sote ni Watanzania, tunajenga nchi yetu, unapambama na serikali kwa ajili gani, kama mlikuwa wanaharakati wa A luta Continua badilikeni, njooni tujenge nchi yetu,” amesema Rais Samia.
Utetezi wa haki za binadamu
Akizungumzia kuhusu utetezi wa haki za binadamu, Rais Samia amewasisitizia wanaharakati wa haki za binadamu kutojihusisha na upande mmoja wa siasa bali kufanyia kazi pande nyingine akitolea mfano haki za panya road na watoto wanaobakwa na kunyanyaswa.
“Watu wanakatwa mapanga na panya roads, sijui kama mmetetea haki zao, mmesema haki zao, zaidi ya kusema polisi wafanye kazi zao lakini je, mmejipangaje kuongea na vijana kuwaelewesha haki za watu na wajibu wao kama vijana wasijiingize kwenye mapanya road,” amesisitiza Rais Samia.
Ushirikiano wa serikali na wanaharakati
Aidha, Rais Samia Suluhu amewaambia wanaharakati kwamba serikali ipo tayari kufanya kazi na taasisi zote kwa kuzingatia haki na kwa lugha nzuri ili kazi iweze kufanyika sawasawa.
“Njoo tushirikiane tufanye kazi, A luta Continua (mapambano yanaendelea), mnapambana na nani? Tena sasa Rais ni Mama, unapambama na mama yako? Na unajua wazi ukipambama na mama yako hata kwa Mungu hupati baraka”- Rais Samia Suluhu Hassan.
Pia, katika maadhimisho hayo Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (TCHRD) umemtunuku tuzo Rais Samia Suluhu kwa kuthamini na kutambua kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha watetezi wa haki za binadamu wanafanya shughuli zao pasipo bughudha yoyote. Tuzo hiyo imetolewa katika maadhimisho ya miaka 10 ya THRDC.