Kuna vitu ambavyo havionekani kwa macho. Inahitaji hisia za moyo na kuzama kwenye ulimwengu wa kufikirika ili kujihisi mnufaika. Mfano hisia ya kupendwa. Kiuhalisia, haihitaji vitu vya kushikika bali ni kushiba kwa nafsi kutokana na umbali ambao mtu anaweza kwenda kuthibitisha kuwa anakupenda.
Pesa, maua, chakula na “viji outing” vinaweza kuwa nyongeza tu lakini mtu kuahirisha kwenda kazini kwa ajili yako, mtu kuachana na pombe ili awe na wewe na mwingine kujiweka mbele yako unapokuwa hatarini, huo ndio upendo. Hivyo basi kama unataka kuingia kwenye mahusiano ni vyema ukazingatia yafuatayo kwa mwenza wako.
- Uhuru wa Kijamii
Mtu sahihi ni yule ambaye utakuwa huru naye kufanya mambo mbalimbali ya kijamii ikiwemo “videti” vya hapa na pale, matembezi, kusapotiana kwenye kazi zenu na pia kukufariji kwenye siku ambazo mambo yanaenda kombo.
- Kuendana mtazamo kwenye mambo mbalimbali
Wakati wewe unaamini hiki, yeye hakiamini na anaamini kile. Ni bora kiwe kitu kimoja lakini vipi kama ni mambo mengi? Mtu ambaye anaweza kukutoa kwenye reli ya mahusiano ni yule ambaye jibu lake ni hapana kwenye kila kitu unachotaka kufanya naye. Iwe kwenda outing, kufanya mazoezi, kuanzisha kitu na kwa baadhi kupiga picha.
- Apite mtihani wa baa
Siyo lazima iwe sehemu ya tungi. Inaweza kuwa sehemu yeyote ya watu wengi. Endapo utakuwa na mtu ambaye kila mara anaangaza angaza pembeni kana kwamba ana hofu ya kufumaniwa, huyo anaweza asiwe mtu wako. Bila shaka mtakuwa wengi kwenye huo moyo wake.
- Awe sikio, bega na hifadhi
Ukiacha kujua rangi unayopenda, chakula unachopenda na tarehe ya kuzaliwa mtu ambaye upo naye kwenye mahusiano anatakiwa kuwa bega lako la kuegemea pale unapohisi dunia inakudondokea pia sikio la kusikiliza matatizo yako pia mtu ambaye upo naye kwenye mahusiano anatakiwa kuwa na shauku ya kukufahamu zaidi. Mwisho kabisa awe mtu mwenye ndoto na anafanya juhudi na mipango ya kuzifikia. Siyo kama mkia kila ulipo na yeye yupo. Katika mahusiano, unahitaji mtu wa kukujenga kimaisha na kuongeza pale wewe unapopungua.