Mshairi nguli kutoka nchini Tanzania Mrisho Mpoto maarufu kwa jina la ‘Mjomba’ amefunguka na kuweka wazi kwamba anasikitishwa na namna baadhi ya wasanii nchini kuimba nyimbo kwa mtindo wa amapiano muziki wenye asili ya Afrika Kusini akidai kwamba kwa kufanya hivyo wasanii wanakua hawaitendei haki tamaduni na muziki wa Tanzania.
Akizungumza kwenye kipindi cha Joto la Asubuhi kinachorushwa na kituo cha televisheni cha TV E, Mpoto alisema ni lazima wasanii wawewazalendo kwa kukuza muziki wa nyumbani na kuuimba kama wanavyoimba nyimbo za mataifa mengine.
“Melody hizi tulizokuwa nazo 164 na zaidi na vikabila vidogovidogo, maproducer na watu wanaoufanya huu muziki wanawezaje kutohoa na kuvunja kama wanavyovunja vitu vingine tukatengeneza aina flani ya mziki au mtu akisika anaona kabisa hii ladha unaipata Tanzania pekee yake,”
“Sasa unakuta mpaka malegendary wakubwa wameingia kwenye amapiano, wote wameingia kwenye amapiano yani ukisikiliza unajiuliza hata huyu anatafuta nini sasa, anatafuta kiki? Anatafuta hela wakati anayo, huyu ndiye angekuwa kioo, huyu ndiye angekuwa njia yakutusaidia kuibua hivi vitu wasanii wengine wakafuata hata yeye kaingia kwenye amapiano, kuna amapiano zimetoka juzi mbili hapa nimeshtuka sana,” alisema Mpoto.
Aidha , Mrisho Mpoto alishauri Wizara ziweke fedha za kufanyika uchunguzi tatizo liko wapi mpaka Tanzania kama nchi inashindwa kupata kitu kitakachokua ni kitambulisho rasmi cha taifa letu.