Mtoto wa Simbachawene asota mahabusu

HomeKitaifa

Mtoto wa Simbachawene asota mahabusu

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, amesema bado wanamshikilia mtoto wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene, huku wakiendelea na kukusanya ushahidi kwa hatua za kisheria zaidi.

Misime alisema, kijana huyo James Simbachawene, anakabiliwa na tuhuma za makosa ya usalama barabarani na kusababisha ajali kwa kuyagonga magari mawili.

Alisema pia kuwa kijana huyo alikuwa mahabusu na wanaendelea kukamilisha ushahidi kulingana na watu walioshuhudia tukio hilo ili hatua za kisheria zichukuliwe.

“Kesho (leo) jalada litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ili asome na kuandaa mashtaka kwa ajili ya kumfikisha mahakamani,” alisema Misime.

Juzi vioande vya video fupi vilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimwonyesha James akibishana na polisi wa usalama barabarani baada ya kudaiwa kusababisha ajali kwa kugonga magari mawili likiwamo Toyota Passo yenye namba za usajili T344 DKG na kujaribu kikimbia kisha akakamatwa.

Muda mchache, ulisambaa ujumbe kwenye mitandao ya kijamii unaoelezwa ni wa Waziri Simbachawene ukisema “Nimeiona clip nakiri ni Kijana wangu ambae ni mtu mzima anajitegemea ana Familia yake, nimemuagiza Mkuu wa Kituo kwa kuwa amekosa adabu kwa Jeshi la Polisi na ametenda kosa, ashughulikiwe bila huruma kwa mujibu wa sheria” 

“Binafsi naomba radhi sana kwa walioathirika na mkasa huo lakini pia kwa Jeshi la Polisi na Watanzania wote poleni kwa usumbufu wowote mlioupata”.

error: Content is protected !!