Mume auwawa kwa kutaka kuongeza mke wa pili

HomeKitaifa

Mume auwawa kwa kutaka kuongeza mke wa pili

Limi Shija (55) mkazi wa Kijiji cha Kabage wilayani Tanganyika mkoani Katavi, anatuhumiwa kwa mauaji ya mume wake Masunga Kashinje (68), kisha mwili wake kuufukia katika shimo la kuchomea mkaa.

Majirani wa famili hiyo, wameeleza familia ya Kashinje ilikuwa kwenye mgogoro wa muda mrefu, baada ya marehemu kudaiwa kwamba anataka kuuza mashamba ya familia yake ili aoe mke mwingine, jambo ambalo lilipingwa vikali na mke na watoto wake.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kabage, Kulwa Mhoja amekiri kutokea kwa tukio hilo ambapo ameeleza kwamba Masunga Kashinje alipotea tangu mwezi Mei mwaka huu, na familia yake ilikuwa ikidai kwamba amesafiri.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, taarifa za mauaji hayo zilianza kusikika Julai 11,2021 ambapo  Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho, alieleza kusikia taarifa kutoka kwa watu waliokuwa katika sherehe ya Kanisa, wakidai kwamba mwili wake upo katika shimo la kuchomea mkaa pembezoni mwa makazi yake.

Viongozi hao wa kijiji pamoja na viongozi wa sungusungu walikwenda kukagua shimo hilo, na kukuta mabaki ya binaadamu, lakini hawakuyaondoa.

Wanadai walikwenda kujadiliana kwani jambo hilo liliwashtua sana.

Baada ya kukaa na taarifa hizo kwa muda mrefu, mwezi Oktoba, iligundulika kwamba mke wa marehemu pamoja na watoto wake, waliondoka kijijini kwao na kuhamia Songea.

Oktoba 10, 2021, Polisi wa Kata walifika kijijini hapo na kuchimba shimo hilo, ambapo walikuta mwili wa binadamu ukiwa umeoza.

Baada ya upelelezi, Novemba 2, 2021, familia hiyo ilirudishwa kijijini hapo ambapo umati mkubwa ulikuwa ukiisubiri familia hiyo.

Mke wa marehemu alidai kwamba, hakuwa na nia ya kumuua mumewe ila alilazimika kuwatumia wauaji ambao awali walitumwa na mume wake ili wamuue yeye.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 55 amedai mumewe alitafuta wauaji na kuwalipa Sh2 milioni ili wamuue yeye (mke) kutokana na ugomvi wa mashamba uliokuwepo kwa muda mrefu, ambapo wauaji walipofika walibaini mkewe huyo hana hana makosa.

Mke anasema aliamua kuwaahidi wauaji kuwa atawaongezea Sh2 milioni ili wamuue mumewe, ambaye ndiye aliwatuma kwake.

“Wauaji walikubali fedha hizo wakamuua mumewe na kumfukia kwenye shimo hilo, baada ya mauaji  Mwenyekiti wa kitongoji alimfuata mtuhumiwa na kumuomba Sh3 milioni ili awapelekee ndugu wa marehemu na kulifanya jambo hilo kuwa siri.

“Alikubali akampa pesa hiyo kufichiwa siri, aligeuka kitega uchumi ambapo viongozi wengine akiwemo wa sungusungu (jina linahifadhiwa) na mjumbe wake nao walimfuata na kumuomba Sh2 milioni ili wamtoroshe,” amesema Mwenyekiti wa Kijiji hicho.

Baada ya mauaji hayo mwanamke huyo aligeuka kitega uchumi, kani inaelezwa kwamba aliwapa viongozi wa sungusungu shilingi milioni 1.4 na wakamsaidia kutoroka.

Kutoka na maelezo hayo, wananchi wenye hasira kali walibomoa nyumba sita ambazo ni makazi ya viongozi waliodaiwa kuchukua fedha kutoka kwa mtuhumiwa ili wafiche siri yake.

Imeelezwa kwamba Polisi waliondoka na mwili wa marehemu na kumshikilia mtuhumiwa huyo pamoja na watoto wake wawili

Chanzo : Mwananchi

error: Content is protected !!