Njia 7 za kuishi na jirani mwenye gubu

HomeElimu

Njia 7 za kuishi na jirani mwenye gubu

Mbali na kuangalia kama mwenye nyumba anaishi eneo hilo hilo unalopanga jambo lingine la muhimu kuzingatia ni aina za majirani wanaokuzunguka.

Kuna sehemu unahamia unakuta jirani ambaye anageuka kuwa mtu wako wa karibu kwingine unakuta jirani ambaye haishwi vimbwanga. Ni vyema kujua jirani yako ni mtu wa namna gani na jinsi ya kuishi nae bila mikwaruzano.

Hakikisha wewe sio jirani mwenye gubu
Ni rahisi kuona tabia za jirani yako zinazokukwaza kuliko kuona tabia zako zinazomkwaza jirani yako. Yawezekana wewe ndio mwenye shida, hivyo hakikisha wewe sio chanzo cha ugomvi kati yako na jirani yako kabla ya kukwazika.

Muziki wako unapiga kwa sauti ya juu sana? Unaamka asubuhi na mapema na kuwapigia kelele majirani zako wakati bado wamelala?

Jua sheria zote za makazi yako
Je! Mwenye nyumba alitoa muongozo wa namna ya kuishi hapo? Una mbwa ilihali sheria za mahali hapo haziruhusu, usafi wa maeneo ya pamoja umnafanywa na nani na kwa utaratibu gani? ama pengine umezidisha idadi ya wageni? Fahamu haya yote kabla ya kuhamia.

Lipa bili zako kwa wakati
Kama mnatumia mita ya maji ama luku kwa pamoja, basi hakikisha unafanya malipo yako kwa wakati, ikibidi andika mahali lini unapaswa kufanya malipo ili usisahau. Ugomvi mwingi wa majirani siku hizi upo kwenye utumiaji wa umeme na maji.

Acha kutengeneza ukaribu sana na jirani
Ndio yawezekana mkatoka kuwa majirani tu na kuishia kuwa marafiki wakubwa. Fanya kazi zako, msalimu na endelea na maisha yako binafsi. Leo ukiomba chumvi ujue kesho ataomba sukari, na kesho kubwa kingine na kingine hivyo jitahidi kuweka mipaka kati yenu.

Katika nyakati zote jiweke mbali na umbea wa kuzungumzia maisha ya watu ama majirani wengine, kumsema mwenye nyumba ama kuambiana siri zenu za ndani. Ikitokea mkawa marafiki wakubwa basi isiwe kwasababu ya umbea.

Acha kuhisi vitu
Kuna jambo linakukera kuhusu jirani yako,mawmbie usihisi kuwa nayeye ana ufahamu sawa na wako na hivyo atajiongeza. Mwambie kistaarabu bila jazba pale unapoona shida na pendekeza namna ya kutatua tatizo hilo.

Weka kumbukumbu zako sawa
Mara ya mwisho umenunua umeme ama maji, hifadhi risiti zako, umelipia usafi ama pesa ya kuzoa taka, hifadhi kumbukumbu zote iwe ni picha, meseji, muda wa tukio fulani, tarehe na hata barua pepe iwapo chochote kitaibuka kuhusu masuala hayo.

Itasaidia pia kutatuamasuala madogo madogo kwa urahisi bila kushirikisha watu wengine. Sio kila unachokiona ni tatizo naye anaona hivyo.

Msikilize anapolalamika kuhusu jambo fulani asilopenda
kama ambavyo kuna mambo yanakukwaza wewe, pengine yapo yanayomkwaza yeye kuhusu wewe na atapokueleza basi sikiliza na kuelewa na kuangalia namna ya kutatua shida hiyo.

Njia gani unatumia kuepuka mikwaruzano na jirani yako?

error: Content is protected !!