Tuzo za Academy maarufu kama (Oscars) zimemfungia muigizaji maarufu wa nchi hiyo Will Smith kutokushiriki tuzo hizo kwa kipindi cha miaka kumi ijayo kutokana na taharuki aliyoleta usiku wa tuzo hizo baada ya kumzaba kibao mchekeshaji Chris Rock jukwaani.
Bodi ya Magavana ilikaa kikao jana Aprili 8 siku 10 kabla ya tarehe ya kikao iliyopangwa huko mjini Los Angeles katika kikao cha dharura baada ya Will Smith kukabidhi barua ya kujitoa kwenye tuzo hizo.
“Bodi imeamua, kwa muda wa miaka 10 kuanzia Aprili 8, 2022, Bw. Smith hataruhusiwa kuhudhuria hafla au programu zozote za Oscars, yeye binafsi au kwa mtandao,” Rais wa tuzo hizo, David Rubin na Mkurugenzi Mtendaji Dawn Hudson walisema katika taarifa iliyotolewa jana.
Smith alipokea matokeo ya bodi hiyo kwa moyo mkunjufu. “Ninakubali na kuheshimu uamuzi wa Academy,” aliiambia CNN.
Barua hiyo iliongeza kuwa: “Tuzo za 94 za Oscar zilikusudiwa kuwasherehekea watu mbalimbali katika jamii yetu ambao walifanya kazi ya kipekee mwaka uliopita; hata hivyo, nyakati hizo zilifunikwa na tabia isiyokubalika na yenye madhara aliyoonesha Smith jukwaani.”
Aidha chuo hicho kilimshukuru Rock kwa namna alivyokabili siku ile “shukrani za dhati kwa bwana Rock kwa kuenzi utulivu wake chini ya hali isiyo ya kawaida.”
Bodi ya Tuzo za Oscars imesema adhabu ya Smith ni njia ya kudumisha nidhamu na usalama wa washiriki wao na watumbuizaji katika sherehe hizo mbalimbali.
Siku iliyofuata baada ya Smith kumpiga kibao Rock kwa kumtania mkewe, Jada Pinkett-Smith katika jukwaa la Oscars alimuomba radhi Rock mtandaoni, alimuomba radhi muandaaji wa tuzo hizo pia.