Rais Samia ahimiza vijana kujiunga na kilimo

HomeKitaifa

Rais Samia ahimiza vijana kujiunga na kilimo

Huenda sekta ya kilimo Tanzania ikachukua sura mpya kwa kuongeza wigo wa ajira pamoja na mchango katika pato la Taifa mara baada ya Serikali kufanya uwekezaji wa mpango wa kilimo cha pamoja (block farms).

Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akizindua mpango wa mashamba ya pamoja jana Machi 10 jijini Dodoma amewataka vijana waliochaguliwa katika mpango huo kufanya kazi kwa bidii kwani Serikali itatoa kila aina ya msaada utakaohitajika.

“Niwaombe sana vijana wangu, watoto wangu mliokubali kuingia kwenye mpango huu, nendeni mkafanye kazi, yale yote tuliyowaahidi kuwapatia, tutawapatia, fanyeni kazi ya kuzalisha mazao ya biashara tuongeze tija kwenye nchi yetu,” amesema Rais Samia.

Pamoja na kuwahimiza vijana, Rais Samia amemtaka Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kusimamia kwa weledi fedha zote zinazotolewa na Serikali kutumika inavyotakiwa katika shughuli iliyokusudiwa ili kuongeza tija.

“Sitavumilia Bashe na wenzio, pale nitakapotoa fedha za wavuja jasho la Watanzania ziende kwenye kilimo zikazalishe, pesa ile ikachezewa, nataka kila shilingi itakayofukiwa kwenye kilimo ikazalishe mara mbili au mara tatu, “ amesisitiza Rais Samia.

Uzinduzi huo wa mpango wa mashamba ya pamoja ambao lengo lake ni kutoa umiliki wa ardhi kwa vijana waliofundwa elimu ya kilimo biashara ili kufanya kilimo chenye tija unafanyika zikiwa zimepita siku tatu tangu Rais Samia alipofungua maandalizi ya Kongamano la Mfumo wa Chakula Barani Afrika jijini Dar es Salaam.

Awamu ya kwanza ya vijana 812 waliochaguliwa kwa ajili ya programu hiyo walianza mafunzo yao Machi 17 ambayo yataendelea kwa muda wa miezi mitatu na kisha kila mmoja atakabidhiwa ardhi isiyozidi ukubwa wa ekari 10 huku Serikali ikifanikisha upatikanaji wa mahitaji mengine ya kilimo.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amewataka vijana wengine zaidi ya 20,000  waliotuma maombi ya kushiriki katika mpango huo kuwa na subira kwani maandalizi ya kuchagua washiriki wengine wa awamu ya pili na ya tatu yanaendelea.

Bashe amebainisha kwamba mpango huo wa mashamba ya pamoja ni miongoni mwa hatua iliyochukuliwa na Serikali ili kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika pato la Taifa kutoka asilimia 26 mwaka 2020 hadi asilimia 36 mwaka 2030.

error: Content is protected !!