Baada ya dosari nyingi kufichuliwa na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/22, watoa maoni mbalimbali wamehusisha hali hiyo na kuongezeka kwa uhuru na uwazi katika kukagua na kuripoti matokeo.
Wamesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ya uwazi zaidi na kukumbatia uwazi jambo lililosababisha kufichua idadi ya hasara katika matumizi ya serikali na makusanyo ya mapato.
Hata hivyo, Rais Samia amepongezwa kwa baadhi ya hatua alizozichukua baada ya uwekaji wazi wa ripoti ya CAG.
Baadhi ya hatua zinazoendelea kuchukuliwa ni kuhakikisha maofisa masuuli wanaandaa majibu ya hoja kama inavyoelekezwa katika Sheria na Kanuni za Ukaguzi wa Umma na kusisitizwa na Rais Samia.
Pia amewakumbusha maofisa masuuli wazingatie maelekezo anayowapa kuhakikisha wanapitia taarifa ya CAG, kujibu na kuchukua hatua za haraka.
WASEMAVYO WADAU
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie, alikuwa na maoni kwamba si kwamba vitendo vya matumizi mabaya ya fedha za umma vimeongezeka katika serikali ya awamu ya sita bali uhuru wa kuripoti matokeo ya ukaguzi umekuzwa.
Hii inatoa fursa kwa CAG kufichua hadharani udhaifu wote uliopatikana wakati wa ukaguzi.
“Hapo awali habari kama hizo zilifichwa, lakini sasa tunaona habari nyingi kwenye uwanja wa umma na watu wanafahamu,” Dk Loisulie alisema.
Aidha alisema Rais Dk Samia Suluhu Hassan amekuwa mwepesi wa kuifanyia kazi ripoti hiyo, kwa uamuzi wake wa kuvunja bodi ya wakurugenzi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) na kutengua uteuzi wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA).
Naye Ellinami Minja, wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), aliyedai kuwa ni muhimu CAG sasa awe na uhuru kama ilivyoainishwa katika sheria.
“CAG amekuwa huru kuchakata taarifa tofauti na awali,” alisema na kuongeza kuwa kutokana na kuongezeka kwa mitandao ya kijamii maudhui ya ripoti hiyo pia yamechapishwa kwa wingi.
Kwa vile uhuru wa vyombo vya habari pia umekuzwa, jambo hilo limewawezesha waandishi wa habari kuripoti tuhuma zilizotolewa na CAG bila hofu ya kufungiwa.
Zaidi ya hayo, Rais Samia anasifiwa na watu wa kawaida ndani na nje ya nchi, hasa nchi jirani, kwa kuchukua hatua za haraka kujibu matokeo ya CAG kuhusu matumizi mabaya ya fedha.
Mbali na kuvunja bodi ya wakurugenzi ya TRC na kutengua uteuzi wa TGFA, Mkuu huyo wa Nchi pia aliagiza Wizara, Makatibu Wakuu kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watendaji waliohusishwa na ripoti hiyo.