Lile agizo alilolitoa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan la kumpatia bajaji mjasiriamali wa lishe, Clara Sanga alilolitoa juzi kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote limetekelezwa kwa haraka na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam.
Hayo yalibainika jana wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam , Amos Makalla alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya uwezeshaji kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 ya makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Temeke.
Akizungumiza agizo la Rais Samia, Makalla alisema wakati wa hafla ya miaka 25 ya mfuko huo, Rais alitembelea mabanda ya wanawake mbalimbali na kukutana na kikundi cha Clara ambacho kilionesha lishe ya wajawazito na jinsi kilivyowapatia wahitaji hospiotalini.
“Rais alifurahi sana akamuagiza mkuu wa mkoa aielekeze Manispaa ya Temeke kupitia fedha hizo inunulie bajaji kikundi cha Imalilo ambacho ni cha Clara,
“Bajaji imenunuliwa kusaidia kikundi hiki kiweze kuhudumia wanawake wajawazito na watoto kwa urahisi. Mnapokabidhiwa mfanye yale mlokusudia,” alisema Makalla.
Clara alimshukuru Rais Samia kwa kumwezesha kupata bajaji hiyo ili imrahisishie upekelekaji wa virutubisho hivyo.
‘Ninamshukuru Mungu, Mkuu wa Mkoa na Halmashauri ya Temeke kwa kuaminiwa na kupewa nafasi na kibali ambacho kimeniwezesha kupita hospitali zote za Temeke kwa watoto na wajawazito,” alisema Clara.