Rais Samia: Siridhishwi na bandari

HomeKitaifa

Rais Samia: Siridhishwi na bandari

Rais Samia Suluhu Hassan amesema haridhishwi na kasi za bandari nchini kutokana na siasa na longolongo zilizopo huku akiwataka watendaji wa bandari kuchapa kazi.

“Siridhishwi kabisa na kasi za bandari zetu, siasa zilizopo, longolongo zilizopo, huko nje bandari zinaendeshwa kwa kasi kubwa sisi bado tunasuasua, wawekezaji wanakuja ni kuzungushwa mwanzo mwisho” amesema Rais Samia Suluhu.

Akizungumza katika hafla ya Utiaji Saini Mkataba wa Ujenzi wa SGR Kipande cha nne (Tabora-Isaka 165KM), Ikulu Dar es Salaam, Rais Samia pia aliweka wazi mpango wa serikali wa kununua vichwa na mabehewa vilivyotumika ili kuanza kutumiwa huku vikisubiriwa vipya vinavyotarajia kupokelewa 2023.

“Tutanunua [vichwa na mabehewa] vya kuanzia vilivyotumika, lakini vyenye hali nzuri, tutavitengeneza reli ifanye kazi. Lakini vipya tulivyoagiza kwa pesa nyingi tutavipokea 2023, na hivyo ndivyo vitakuja kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi.”- amesema Rais Samia Suluhu.

Aidha, Rais Samia amewataka wananchi kwa ujumla na wasimamizi wa miradi kuwa makini na miradi hiyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha miundombinu inasimamiwa vizuri na kulindwa ili iweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu.

 

error: Content is protected !!